Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kupitia banda lake katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Katika maonesho hayo, maafisa wa THBUB wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu, wajibu wa kila mwananchi katika kuheshimu na kulinda haki hizo, pamoja na nafasi ya Tume katika kukuza na kulinda haki za binadamu na kuimarisha misingi ya utawala bora nchini.
Aidha, wananchi wanaotembelea banda la THBUB wanapata fursa ya kufahamu majukumu ya Tume, taratibu za kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, pamoja na kupata ushauri na ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume.
THBUB imeendelea kuwahamasisha wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Nanenane kutembelea banda lake ili kujifunza zaidi kuhusu haki zao, kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kushiriki katika kujenga jamii inayozingatia haki, usawa na utawala bora.
Ushiriki wa THBUB katika Maonesho ya Nanenane ni sehemu ya juhudi za kuifikia jamii kwa karibu na kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu haki za binadamu na huduma zinazotolewa na Tume, kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.





No comments:
Post a Comment