📍Dodoma
Tume ya Madini imesema inatumia Maonesho ya Nane Nane mwaka 2026 kama jukwaa la kuhamasisha uwekezaji na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kupitia utoaji wa elimu kuhusu fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuanzia utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani, biashara ya madini sambamba na ushiriki wa watanzania katika sekta hiyo.
Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, leo Agosti 3, 2026, Meneja Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema ushiriki wa Tume unalenga kuwafikia wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali kwa kuwapatia elimu sahihi itakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za madini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Amesema mbali na kutoa elimu kuhusu uwekezaji, Tume inaendelea kuhamasisha wachimbaji na wananchi kuzingatia usalama migodini kwa kutoa elimu ya kinga dhidi ya ajali, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga, utunzaji wa mazingira na uzingatiaji wa kanuni za afya na usalama mahali pa kazi.
Mwase amesema banda la Tume ya Madini limeandaliwa mahsusi kuwa kituo cha elimu ambapo wananchi wanapata maelezo ya kitaalamu kuhusu huduma zinazotolewa na Tume, masharti ya kupata leseni mbalimbali za madini, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma, pamoja na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta hiyo.
“Maonesho haya yanatupatia fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi, kujibu maswali yao na kuwaelekeza namna bora ya kushiriki katika Sekta ya Madini kwa njia halali na yenye tija kwao na kwa Taifa,” amesema Mwase.
Ameongeza kuwa ushiriki wa Tume katika Maonesho ya Nane Nane unaendana na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” kwa kuwa unachochea uelewa wa wananchi kuhusu fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za madini na mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amewahimiza wananchi, wachimbaji, wafanyabiashara wa madini, wanafunzi na wawekezaji kutembelea banda la Tume ya Madini ili kupata elimu, ushauri wa kitaalamu na taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume pamoja na fursa zinazopatikana katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Tume ya Madini imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, ikiwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za madini nchini, ikiwemo utoaji wa leseni za madini, ukaguzi wa shughuli za uchimbaji, usimamizi wa biashara ya madini, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na utoaji wa elimu kwa wadau.
Katika kutekeleza jukumu la kuelimisha umma, Tume inaendelea kutumia mikakati mbalimbali ya mawasiliano ikiwemo ushiriki katika maonesho ya kitaifa na kimataifa, makongamano, semina, mikutano ya wadau, vipindi vya redio na televisheni, machapisho mbalimbali, tovuti, pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu Sekta ya Madini, fursa za uwekezaji na ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Tume ya Madini inaongozwa na Dira ya kuwa mdhibiti wa Sekta ya Madini wa kiwango cha kimataifa anayesimamia uchimbaji endelevu wa madini unaochochea maendeleo ya viwanda na ustawi shirikishi kwa wote.
Aidha, Dhima yake ni kusimamia na kudhibiti Sekta ya Madini kwa uwazi kupitia usimamizi na ufuatiliaji madhubuti, huku ikihamasisha utafutaji wa madini, uchimbaji, uongezaji thamani wa madini na biashara ya madini kwa ajili ya maendeleo endelevu.





No comments:
Post a Comment