"UKARABATI WA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA WAFIKIA ASILIMIA 67" WAZIRI MBARAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 18, 2026

"UKARABATI WA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA WAFIKIA ASILIMIA 67" WAZIRI MBARAWA


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma umefikia asilimia 67 na unatarajiwa kukamilika Desemba 5, 2026, hatua inayolenga kuimarisha huduma za usafiri wa anga na kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani humo

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 15, 2026, wakati akikagua maendeleo ya mradi huo, Prof. Mbarawa amesema mradi wenye thamani ya Shilingi bilioni 51.4 ulianza mwaka 2023 na umeendelea kwa kasi, ambapo utekelezaji umeongezeka kutoka asilimia 61 hadi 67 ndani ya mwezi mmoja.

Amesema asilimia 80 ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya ukarabati vimekwishawasili uwanjani, huku vifaa vilivyosalia vikiwa ni taa za kuongozea ndege, ambazo zinatarajiwa kufika ndani ya miezi miwili, sambamba na kipindi cha kukamilika kwa mradi huo.

Kuhusu utekelezaji wa kifedha, Waziri Mbarawa amesema mkandarasi tayari amelipwa Shilingi bilioni 23, huku hati nyingine ya malipo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.23 ikiwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kukamilisha malipo kwa mkandarasi.

Prof. Mbarawa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo Kigoma, na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya uchukuzi ili wananchi wapate huduma za usafiri wa kisasa, salama na zenye ufanisi

Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Rashid Chuachua amemshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha za mradi huo na kumpongeza Waziri Mbarawa kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa miradi ya maendeleo mkoani humo

amesema uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya anga, reli na usafiri wa majini umeifanya Kigoma kubadilika kutoka kuwa “mwisho wa reli” na kuwa eneo linalofungua fursa mpya za biashara, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia miradi hiyo kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo katika Ukanda wa Magharibi.

Awali Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma Mha. Elison Mweladzi alimhakikishia Waziri Mbarawa kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea kwa weledi na utakamilika kwa wakati kwa maslahi ya wanakigoma na Taifa.

No comments:

Post a Comment