
Na Okuly Julius – OKULY BLOG, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeanza rasmi kuwalipa fidia wananchi 880 wa vitongoji vya Mpera na Sokoine wilayani Chamwino, mkoani Dodoma, kiasi cha shilingi bilioni 4.928, ili kupisha na kulinda eneo la hifadhi ya chanzo cha maji cha Bonde la Chamwino.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mingi kati ya wananchi na Serikali, huku ikilenga kuhakikisha chanzo hicho kinahifadhiwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji ya uhakika na endelevu kwa wakazi wa Dodoma.

Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Chamwino wakati wa hafla ya kuwasilisha malipo hayo leo Agosti 18,2026, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kutambua umuhimu wa chanzo hicho katika kukidhi mahitaji ya maji yanayoongezeka katika Jiji la Dodoma.
Amesema tangu Serikali ilipohamia Dodoma mwaka 2017, mahitaji ya maji yameongezeka kwa kasi kutoka lita milioni 45 kwa siku hadi lita milioni 159 kwa siku, wakati uzalishaji wa sasa ukiwa takribani lita milioni 88 kwa siku.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, hali hiyo inaifanya hifadhi ya vyanzo vya maji kuwa jambo la msingi katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika, hususan wakati mahitaji yakiendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.
Kundo amesema eneo la Bonde la Chamwino lilitengwa tangu kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, lakini mchakato wa kuwalipa wananchi walioathiriwa umefanikishwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema eneo hilo lilitengwa awali likiwa na ukubwa wa takribani ekari 740, ambapo kati ya mwaka 1970 na 1980 Serikali ilichimba mabwawa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima na wafugaji.
Amesema baada ya Dodoma kutangazwa kuwa makao makuu ya nchi mwaka 1973, mahitaji ya maji yaliongezeka na eneo la hifadhi likapanuliwa hadi kufikia takribani ekari 2,100, hatua iliyohusisha maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na wananchi na baadaye kusababisha migogoro ya ardhi.
Mhandisi Waziri alisema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maji iliunda timu ya wataalamu iliyofanya tathmini na kupendekeza Serikali izingatie eneo la awali la ekari 740 katika hatua za kulinda chanzo hicho.
Amesema mchakato wa uthamini wa ardhi na mali ulianza rasmi Agosti 2024, ukihusisha wananchi kupitia mikutano ya kutoa elimu pamoja na uwekaji wa mipaka ya eneo hilo.
Aidha, amefafanua kuwa fidia hiyo inalipwa kwa wananchi waliothibitika kuathirika na eneo la hifadhi, huku taasisi za Serikali kama shule na miradi mingine ya umma zikishughulikiwa kupitia utaratibu mwingine wa Serikali.
FIDIA YAFIKIA SH. BILIONI 36.5 NCHI NZIMA
Wizara ya Maji imeeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 36.5 kulipa fidia katika maeneo 21 ya vyanzo vya maji nchini.
Fedha hizo zimewanufaisha jumla ya wananchi 11,731 waliopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, amesema kuanza kwa ulipaji wa fidia ni hatua muhimu katika kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mingi na kuathiri zaidi ya wananchi 800.
Mayanja amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za fidia na kueleza kuwa Serikali imefanikiwa kufuta kero ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.
Amewataka wananchi kutumia fedha watakazopokea kwa busara, ikiwemo kutafuta maeneo mbadala ya shughuli zao za kilimo, ili fidia hiyo iwe na manufaa ya muda mrefu kwa familia zao na kuepusha migogoro mipya.

Naye mwananchi wa Chamwino, Eliesa Nyembela, alisema wananchi wamepokea hatua hiyo kwa furaha baada ya kusubiri kwa muda mrefu tangu mwaka 1996.
Nyembela aliishukuru Serikali na viongozi mbalimbali kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kufuatilia suala hilo hadi kufikia muafaka, huku akiwataka wananchi wenzao kuendelea kudumisha amani na kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya familia zao.
Katika maelekezo yake, Naibu Waziri Kundo Mathew amezitaka Bodi za Maji za Mabonde kuhakikisha maeneo yote ya vyanzo vya maji yaliyolipiwa fidia yanalindwa, yanawekewa mipaka na kutangazwa rasmi kuwa maeneo ya hifadhi.
Pia, mamlaka za maji zimetakiwa kushirikiana kwa karibu na bodi hizo katika kulinda vyanzo hivyo, huku zikitakiwa kuratibu upatikanaji wa hati miliki za maeneo ya miundombinu na vyanzo vya maji ili kuzuia migogoro ya ardhi siku zijazo.
Aidha, Bodi za Maji za Mabonde zimetakiwa kufanya tathmini ya maeneo yote ya vyanzo vya maji ili kubaini kiwango cha uvamizi na uharibifu wa mazingira na kuweka mikakati madhubuti ya kuyahifadhi.
Kundo alisisitiza kuwa maji ni mali ya umma na kwamba ulinzi wa vyanzo vyake ni wajibu wa kila mwananchi, akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali kuhakikisha maeneo ya hifadhi hayavamiwi wala kuharibiwa.
Kwa upande wa Wizara ya Maji, hifadhi ya Bonde la Chamwino inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika na endelevu kwa wakazi wa Dodoma, pamoja na kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Miji 28 kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.










No comments:
Post a Comment