WORLDSKILLS TANZANIA, ENABEL YAONGEZA NGUVU KWA VIJANA WENYE VIPAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 21, 2026

WORLDSKILLS TANZANIA, ENABEL YAONGEZA NGUVU KWA VIJANA WENYE VIPAJI

 


Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) limesema litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha vijana wanaoshiriki Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi WorldSkills Tanzania 2026 wanapata fursa za ajira na kufikia ushindani wa kimataifa.


Akizungumza leo Agosti 21,2026 katika maonesho ya kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya shule ya sekondari Usagara jijini Tanga Mwakilishi wa Enabel nchini, Abel Mbilinyi amesema shirika hilo ni miongoni mwa wadhamini wa mashindano hayo kwa kutoa vifaa vya mashindano, zawadi kwa washindi na kumleta mtaalamu kutoka Ubelgiji kwa ajili ya kujenga uwezo wa waandaaji na majaji.


Mbilinyi amesema Enabel imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira kupitia ushirikiano na taasisi za mafunzo ya ufundi ikiwemo VETA na taasisi nyingine za elimu ya ujuzi.


"Lengo kuu la shirika letu ni kuhakikisha vijana wanapata ajira za staha, huku wengine wakipewa uwezo wa kujiajiri kupitia ujuzi walioupata,"amesema.


Kwa mujibu wa Mbilinyi, maelfu ya vijana tayari wamenufaika na programu za Enabel ambapo wengi wamepata ajira huku wengine wakianzisha shughuli zao za kiuchumi.


Ameongeza kuwa washindi wa WorldSkills Tanzania 2026 hawataishia kwenye mashindano ya kitaifa, bali Enabel itaendelea kuwasaidia kuelekea mashindano ya Afrika na baadaye ya dunia yatakayofanyika nchini China.


Mbilinyi amesisitiza kuwa ushirikiano na sekta binafsi utaendelea kuimarishwa ili kuwaunganisha vijana wenye vipaji na waajiri, hatua itakayowawezesha kutumia ujuzi wao kujenga maisha na kuchangia uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment