Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Hati Fungani Tanga ametakiwa kuhakikisha anafanya kazi kwa saa 24 ili mradi ukamilike.
Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) ametoa maelekezo hayo akikagua mradi wa Hati Fungani Tanga unaoendelea katika eneo la Moe.
"Hatuna muda wa kupoteza, mkandarasi shinda eneo la kazi, Fedha ipo, hadi Novemba 2026 mradi uwe umekamilika na wananchi waanze kupata maji ya mradi huu," Aweso amesema
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kwamba Taasisi za serikali ziwe na vyanzo mbadala vya fedha katika kutoa suluhu ya changamoto za watu, na kusema huu ni mradi wa mfano wa chanzo mbadala cha fedha na usimamizi wake usiwe wa kawaida na viongozi wanautemembelea mara kwa mara na kuahidi kuwa atarudi tena Oktoba 2026 ili kuhakikisha kazi inakamilika.
Mradi wa uboreshaji miundombinu ya maji wa Hati Fungani ya Kijani ya Tanga UWASA unathamani ya Shilingi bilioni 53.12 ambapo mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefika zaidi ya asilimia 72 na utaanza kutoa huduma kwa wakazi wa Tanga Jiji, Muheza, Mkinga na Pangani mapema Novemba 2026.
Mradi wa Maji huo unajumuisha upanuzi wa mtandao wa mifumo ya majitaka katika Jiji la Tanga, ubadilishaji wa kilomita 110 za mabomba chakavu ya maji, ufungaji wa Dira elfu 10 za malipo kwanza, upanuzi wa mtambo wa usambazaji maji kutoka Lita Milioni 45 Hadi kufikia Lita Milioni 60 kwa siku sambamba na ujenzi wa Tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita milioni 35 ambapo itafanya maeneo yote ya Tanga Jiji, Muheza, Mkinga na Pangani kupata maji saa 24.








No comments:
Post a Comment