Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinakutana jijini Dar es Salaam kujadili na kuweka mikakati ya kutatua changamoto na vikwazo vinavyokwamisha biashara ndani ya Jumuiya, hususan Vikwazo Visivyo vya Kikodi (Non-Tariff Barriers – NTBs).
Mkutano huo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi za EAC, uliofanyika jijini Arusha Machi 7, 2026, ambao ulizitaka Nchi Wanachama kuchukua hatua za haraka za kuondoa vikwazo vyote vya biashara visivyo vya kodi vilivyoripotiwa ndani ya Jumuiya ifikapo Juni 30, 2026.
Sanjari na hayo, mkutano huo utajadili hatua za utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano Maalum wa Pili wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi (SCFEA) uliofanyika Novemba 25, 2025, ambao ulielekeza nchi wanachama kuondoa ushuru, ada, tozo na kodi za ndani zinazobagua bidhaa za Nchi Wanachama kinyume na matakwa ya Ibara ya 10 na 15 ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya EAC, ifikapo Juni 30, 2026 na kufanya marekebisho ya tafsiri ya baadhi ya maneno katika sheria za ndani ili kuendana na makubaliano ya Jumuiya.
Miongoni mwa ajenda muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na; tathmini ya utendaji wa Vituo vya Pamoja vya Huduma Mpakani (One Stop Border Posts – OSBPs), Mpango Kazi wa Kutatua Masuala Yanayoathiri Biashara ndani ya Jumuiya, pamoja na Jedwali la Utekelezaji wa Mpango Kazi huo.
Mkutano huo pia utajadili na kupitia Orodha ya Vikwazo Visivyo vya Kodi (Non-Tariff Barriers Index) ya EAC, ambayo ni miongoni mwa nyenzo zinazotumika kufuatilia, kutambua na kupima hatua zinazochukuliwa na Nchi Wanachama katika kushughulikia vikwazo vinavyoathiri biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Soko la Pamoja la EAC, ambalo linalenga kurahisisha usafirishaji bidhaa, watu, huduma na mitaji na haki ya kuanzisha shughuli za biashara katika Nchi Wanachama. Kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kodi na kurahisishwa kwa taratibu za mipakani kunatarajiwa kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara, kuongeza ushindani na kukuza biashara ya ndani ya Jumuiya.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo na hatua mahususi za utekelezaji zitakazosaidia kuharakisha uondoaji wa vikwazo vya biashara, kuboresha ufanisi mipakani na kuimarisha biashara ya kikanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za EAC kujenga Jumuiya yenye ushindani, jumuishi na inayotoa fursa zaidi kwa wananchi wake.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ngazi ya Wataalamu unaongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga, akiongozana na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.








No comments:
Post a Comment