NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeanzisha programu mbili mpya za shahada zinazolenga kuwaandaa vijana kuwa wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa, teknolojia na uwezo wa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
Programu hizo ni Shahada ya Usimamizi wa Biashara kwa mfumo wa Double Degree na Shahada ya Usimamizi wa Suluhisho za Kidijitali na Teknolojia kwa mfumo wa Uanagenzi (Apprenticeship).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Septemba 14, 2026, Mkuu wa CBE, Prof. Edda Lwoga, amesema programu ya Double Degree inatolewa kwa ushirikiano na Southern West University of Finance and Economics (SWUFE) ya China.
Amesema mwanafunzi atatumia miaka miwili kusoma Tanzania na miaka miwili China, huku akipata shahada kutoka CBE na SWUFE.
Kwa mujibu wa Prof. Lwoga, programu hiyo inalenga kuzalisha mameneja na viongozi wenye uwezo wa kusimamia biashara za ndani na kimataifa, pamoja na kuwawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa mazingira ya biashara ya kimataifa.
“Programu hii itawawezesha wahitimu kupata ujuzi wa kupanga, kuongoza na kusimamia biashara za ndani na za kimataifa kwa ufanisi,” amesema.
Amesema programu hiyo pia itaongeza fursa kwa wahitimu katika soko la ajira ndani na nje ya nchi, kutokana na kupata elimu na uzoefu wa kimataifa.
Akizungumzia programu ya pili, Prof. Lwoga amesema Bachelor Degree in Digital and Technology Solutions Management with Apprenticeship inalenga kuwaandaa vijana kutumia teknolojia za kidijitali kutengeneza suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na Taifa.
Amesema programu hiyo itatolewa kwa mfumo unaomuwezesha mwanafunzi kusoma darasani kwa muhula mmoja na kutumia muhula mwingine kujifunza kwa vitendo katika mazingira halisi ya kazi.
Amesema mfumo huo utasaidia kuunganisha elimu ya darasani na uzoefu wa kazi, hivyo kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Programu hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya CBE na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) baada ya taasisi hizo kusaini makubaliano ya ushirikiano.
“Faida kubwa ya programu hii ni kuwaandaa vijana kuwa wataalamu wa teknolojia na suluhisho za kidijitali, jambo ambalo ni muhimu sana katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa CBE upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Robert Mashenene, amesema chuo hicho kimefanikiwa kuwaendeleza wabunifu zaidi ya 300.
Amesema kati yao, wabunifu sita wameshiriki katika mashindano ya ubunifu nchini, huku baadhi ya bunifu zao zikichukuliwa na Wakala wa Vipimo (WMA) kwa matumizi ya kupima magari yanayosafirisha mafuta.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Machapisho na Ushauri wa Kiuchumi wa CBE, Prof. Nasibu Mramba, amesema chuo hicho kinaendelea na tafiti saba, zikiwemo zinazohusu urasimishaji wa biashara na changamoto ya wataalamu wanaotumika katika viwanda.
Prof. Lwoga amewataka vijana na Watanzania kutumia fursa za programu hizo, akisema dirisha la udahili kwa mwezi Septemba limefunguliwa.

No comments:
Post a Comment