MAKONDA HATAMBUI JEZI MPYA ZA TIMU YA TAIFA, AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA MIKATABA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 18, 2026

MAKONDA HATAMBUI JEZI MPYA ZA TIMU YA TAIFA, AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA MIKATABA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, ametangaza kutoutambua mchakato wa kubadilisha jezi za timu za taifa, akisema umefanyika bila kuishirikisha Wizara licha ya maelekezo aliyoyatoa Februari 2026.

Sambamba na hatua hiyo, Waziri Makonda ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu itakayochunguza mikataba ya wazabuni wa jezi hizo, manufaa yake kwa timu za taifa pamoja na mapato yatokanayo na mauzo ya jezi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo leo, Septemba 18, 2026, uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo mikataba iliyopo inanufaisha timu za taifa kwa kiwango kinacholingana na fedha nyingi zinazotolewa na Serikali kugharamia timu hizo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Februari 2026, Waziri Makonda alitoa maelekezo ya kuboresha jezi za timu za taifa ili ziakisi utambulisho wa Tanzania na kuzalisha manufaa mapana zaidi kwa nchi.

Hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027 (AFCON 2027).

Wizara imebainisha kuwa jezi za timu za taifa hazipaswi kuangaliwa kama mavazi ya wachezaji pekee, bali pia kama sehemu ya utambulisho wa taifa na chanzo cha mapato yanayoweza kusaidia uendeshaji wa timu hizo.

“Pamoja na kutoutambua utambulisho wa jezi za timu ya taifa, Waziri Makonda ataunda Kamati ya kuchunguza mikataba ya mzabuni wa jezi hizo, ili kubaini manufaa ya mikataba hiyo kwa timu za taifa ambazo zimekuwa zikigharimiwa na Serikali kwa fedha nyingi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi Zaituni Mkwama. 

Kamati hiyo pia itachunguza namna mapato yanayotokana na mauzo ya jezi za timu za taifa yanavyokusanywa na mchango wake katika kugharamia shughuli za timu hizo.

No comments:

Post a Comment