Ziara hiyo imekuwa ya aina yake baada ya Mhe. Mhando kuonyesha kwa vitendo mshikamano na wananchi katika kusukuma maendeleo, ikiwemo kubeba mwenyewe mifuko ya saruji mabegani kuelekea eneo la ujenzi wa Zahanati ya Pagwi.
Katika ujenzi huo unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi, Mhe. Mhando alikabidhi mifuko 50 ya saruji pamoja na Sh500,000 taslimu kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi huo.
Mbunge huyo pia aliahidi kuongeza mifuko mingine 100 ya saruji, akisema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya kukamilika kwa zahanati hiyo na kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya karibu na makazi yao.
Zahanati hiyo inatarajiwa kupunguza adha ya wananchi wa Pagwi ambao wamekuwa wakilazimika kusafiri hadi Lumotio kufuata huduma za afya.
Akizungumza na wananchi wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mhando alisema ataendelea kuifuatilia Kata ya Pagwi na kusukuma mbele hoja za maendeleo, akisisitiza kuwa changamoto za wananchi zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua.
“NITAITIFUA TIFUA PAGWI HADI KIELEWEKE,” alisema Mhe. Mhando, akiahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu masuala ya maendeleo katika kata hiyo.
Alitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na barabara, maji, umeme, afya na madaraja, akisema miundombinu bora ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na shughuli zao za kiuchumi.
BARABARA SUNYA–PAGWI–MAKELELE
Mhe. Mhando pia alizungumzia changamoto ya barabara ya Sunya–Pagwi–Makelele, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuifuatilia ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwa wananchi.
Aidha, aligusia changamoto ya Daraja la Makelele, linalounganisha maeneo ya Lumotio na Makelele, akisema wakati jitihada za kupata daraja la kudumu zikiendelea, ni muhimu kutafutwa kwa haraka kwa daraja la muda ili wananchi wasikwame katika shughuli zao.
Alisema pia kuna umuhimu wa kuendelea kufungua mawasiliano ya barabara katika njia za Sunya–Lumotio–Makelele–Sambu–Songe, pamoja na Kikunde–Chamtui–Lumotio–Sunya.
UMEME WAFIKA MALALI NA MASIMBA
Katika sekta ya umeme, Mhe. Mhando alisema maeneo ya Malali na Masimba tayari yamefikiwa na huduma hiyo, huku akisisitiza kuwa jitihada zitaendelea ili maeneo mengine nayo yaunganishwe na umeme.
ATOA SHILINGI MILIONI MOJA UJENZI OFISI YA KIJIJI.
Akiwa katika Kijiji cha Chamtui, Mhe. Mhando alitoa Sh 1 milioni kwa ajili ya ununuzi wa bati zitakazotumika katika upauaji wa jengo la Ofisi ya Kijiji hicho.
Mbali na hilo, alilipia ada vijana watano kutoka Chamtui kwenda kupata mafunzo ya ufundi katika Chuo cha VETA, hatua inayolenga kuwawezesha kupata ujuzi wa kuwaongezea fursa za kujiajiri na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
MICHEZO YAPATA MSUKUMO
Mhe. Mhando pia alitoa jezi kwa timu mbalimbali za soka katika maeneo aliyotembelea, zikiwemo Lipuli FC ya Chamtui, Mikocheni FC ya Mtakuja, Azam FC ya Chang’ombe na Toto FC ya Nyamaleni.
Aidha, alikabidhi jezi kwa timu mbili za Kijiji cha Pagwi pamoja na jozi moja kwa ajili ya wanafunzi.
WANANCHI TUMEONA JITIHADA ZA MBUNGE WETU
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Pagwi walimshukuru Mhe. Mhando kwa kuwafikia, kuwasikiliza na kushirikiana nao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Walisema wamefarijika kuona Mbunge wao akijikita katika masuala yanayogusa maisha yao moja kwa moja, yakiwemo afya, barabara, maji, umeme, madaraja, elimu na fursa kwa vijana.
Wananchi hao pia walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Ziara ya Mhe. Mhando katika Kata ya Pagwi imeweka msisitizo katika ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maendeleo, huku ahadi na michango iliyotolewa ikitarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa baadhi ya miradi katika eneo hilo.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)



No comments:
Post a Comment