
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imewataka wataalam wa Ununuzi na Ugavi ambao hawajalipa ada zao za mwaka kulipa madeni yote ndani ya siku 30, vinginevyo usajili wao unaweza kufutwa na majina yao kuchapishwa rasmi.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 14,2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo , Godfred Mbanyi, ambapo walijadili amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wataalam wote wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Bodi.
Mbanyi amesema mtaalam yeyote ambaye hatalipa ada ndani ya muda uliowekwa anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwemo kufutiwa mara moja usajili wake.
Ameeleza kuwa kila mtaalam aliyesajiliwa anawajibika kulipa ada ya mwaka kwa mujibu wa kiwango kinachowekwa na Bodi.
Aidha, Mbanyi amesema mtaalam ambaye atashindwa kulipa ada kwa kipindi cha miezi 24 mfululizo, atachukuliwa kuwa amepoteza hadhi ya usajili na jina lake linaweza kuondolewa kwenye daftari rasmi la usajili la PSPTB.
Amesisitiza kuwa mtu yeyote atakayeendelea kufanya kazi, kujitambulisha au kujihusisha na taaluma ya Ununuzi na Ugavi bila kusajiliwa na PSPTB, atakuwa ametenda kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.
PSPTB imewataka wataalam wenye madeni kuchukua hatua za haraka na kuhakikisha wanakamilisha malipo ndani ya siku 30.

No comments:
Post a Comment