Na OWM-TAMISEMI, Dodoma
Timu ya wanamichezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, imeondoka kuelekea mkoani Kilimanjaro ikiwa na dhamira ya kufanya vizuri na kurejea na vikombe katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanamichezo hao Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa OWM-TAMISEMI, Bw. Adolf Ndunguru, amewataka wanamichezo wote wa ofisi yake kucheza kwa ari, nidhamu na mshikamano ili kuiwakilisha vyema Ofisi katika mashindano hayo.
“Nendeni mkashindane kwa moyo mmoja, mshirikiane na muwe na nidhamu. Kila mmoja wenu ni mwakilishi wa TAMISEMI; tunatarajia kuona juhudi na kujituma ili mpate ushindi na kurejea na vikombe,” amesema Bw. Ndunguru.
Ameongeza kuwa mafanikio katika michezo yanahitaji ushirikiano wa timu, kuheshimu wapinzani na kuzingatia sheria na kanuni za mashindano. Amewahimiza wanamichezo na Viongozi wao kudumisha umoja katika kipindi chote watakachokuwepo mkoani Kilimanjaro.
Katika mashindano hayo, OWM-TAMISEMI itachuana katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, karata, bao na darts. Ushiriki huo unalenga kukuza vipaji na kuimarisha afya miongoni mwa watumishi wa Ofisi hiyo.
Mashindano ya SHIMIWI huwakutanisha watumishi kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali, yakitoa nafasi ya kuimarisha afya, mshikamano, ushirikiano na mahusiano ya kikazi kupitia michezo na burudani.





No comments:
Post a Comment