WATAALAMU 22 WA AFRIKA NA NJE YA AFRIKA WAKUTANA DAR KUJADILI MITAALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 22, 2026

WATAALAMU 22 WA AFRIKA NA NJE YA AFRIKA WAKUTANA DAR KUJADILI MITAALA

Tanzania imefungua milango kwa wataalamu wa elimu kutoka ndani na nje ya Afrika kujadili namna ya kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa ya wanafunzi, jamii na soko la ajira.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Sita la African Curriculum Association Conference jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho yanayofanyika katika sekta ya elimu.

Prof. Shemdoe amesema wajumbe kutoka nchi 22 wameshiriki kongamano hilo, likiwakutanisha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Ubelgiji, Uingereza na Marekani.

Amesema mjadala mkubwa katika kongamano hilo unalenga kuangalia namna elimu inavyoweza kumjengea mwanafunzi uwezo wa kutumia maarifa katika kutatua changamoto za maisha, badala ya kutegemea zaidi nadharia.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mabadiliko hayo unaenda sambamba na uwekezaji katika mazingira bora ya kujifunzia, akitaja ujenzi wa shule 130 za awali kama sehemu ya hatua zinazochukuliwa.

Kwa mujibu wa Prof. Shemdoe, maboresho hayo yanahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Mwanakhamisi Adam Ameir, amesema kongamano hilo limeipa Tanzania na Zanzibar fursa ya kujifunza namna nchi nyingine zinavyokabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mabadiliko ya mitaala.

Amesema mtaala unaotekelezwa tangu mwaka 2023 umejikita pia katika maeneo ya teknolojia na elimu ya amali, kwa lengo la kuwajengea vijana ujuzi unaoweza kutumika katika maisha ya kila siku na katika soko la ajira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba, amesema mjadala huo unalenga pia kuhimiza nchi za Afrika kuwa na mitaala inayozingatia utambulisho, historia, tamaduni na mazingira ya bara hilo.

Dkt. Komba amesema Afrika inahitaji kuendelea kujenga mifumo ya elimu inayozingatia mahitaji ya Waafrika na mazingira wanayoishi, huku ikihakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaowawezesha kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.

Kongamano hilo litafanyika kwa siku nne na linatarajiwa kuzaa Azimio la Dar es Salaam kuhusu mitaala ya Afrika, mwongozo wa uundaji wa mitaala pamoja na mapendekezo ya utekelezaji.

Aidha, washiriki wanatarajiwa kutembelea shule siku ya mwisho ya kongamano hilo ili kujionea kwa vitendo utekelezaji wa maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu.


No comments:

Post a Comment