Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam .
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinazohusika na Mafuta na Gesi Asilia ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.
Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 5, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Homera amepokea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya mafuta na gesi asilia.
Aidha kikao hicho kimejadili kwa kina masuala yanayohusu upatikanaji na usalama wa mafuta nchini, usimamizi wa shughuli za mafuta na gesi asilia, pamoja na kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katika kikao hicho, Waziri Homera amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara, akieleza kuwa sekta ya mafuta na gesi ni muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya Taifa.
Ameelekeza taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika, kwa wakati na kwa bei inayozingatia maslahi ya wananchi, sambamba na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya Taifa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Mafuta, Bw. Goodluck Shirima; pamoja na viongozi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).









No comments:
Post a Comment