
NA ERICK NENDA, OKULY BLOG, DODOMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imewasogezea wananchi huduma mbalimbali katika maeneo yao, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yanayoanza leo Oktoba 5 hadi 9, 2026.
Hatua hiyo inalenga kuwafikia wateja moja kwa moja katika maeneo wanayoishi na kufanyia shughuli zao, kuwasaidia kutatua changamoto za huduma za maji pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kulazimika kufika katika ofisi za DUWASA.
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa DUWASA, Lenar Mwakisale, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “The Extra Mile”, inayolenga kuhimiza utoaji wa huduma unaokwenda zaidi ya matarajio ya mteja.
Amesema DUWASA imejipanga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi walipo, badala ya kusubiri wateja wafike katika ofisi za mamlaka hiyo.
“The Extra Mile maana yake ni kwenda beyond what a customer expected. Katika hilo, tumejipanga kuhakikisha tunawafikia wateja wetu popote pale walipo ili tufanye zaidi ya matarajio yao, zaidi ya vile ambavyo wamezoea,” amesema Mwakisale.
Amesema katika kipindi cha wiki hiyo, DUWASA imeweka vituo maalumu vya huduma katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma, ikiwemo Msalato, Veyula, Nzuguni na Nkuhungu, kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa urahisi na kutatua changamoto zao kwa wakati.
Kwa mujibu wa Mwakisale, mpango huo pia unahusisha kuwafikia wananchi katika maeneo yenye shughuli nyingi, ikiwemo Machinga Complex na Stendi ya Nane Nane, ambako wananchi wengi hufanya shughuli zao za kila siku.
Amesema hatua hiyo imekuja baada ya DUWASA kubaini kuwa wananchi wanahitaji huduma zilizosogezwa karibu nao, huku ziara za maeneo mbalimbali zikitoa fursa kwa mamlaka hiyo kujionea changamoto zinazowakabili wateja.
“Kikubwa ambacho tume-notice ni kwamba wateja wanatamani sana tuweke ukaribu. Kwa ukaribu tulioonyesha leo, inawezekana ndiyo mwanzo wetu wa kusogeza huduma katika maeneo ambayo ofisi zetu zipo mbali kidogo,” amesema Mwakisale.
Aidha, amesema DUWASA imejipanga kuwasaidia wateja wenye changamoto mbalimbali za huduma, ikiwemo madeni ya maji, kwa kuwafikia walipo na kuwasaidia kupata ufumbuzi unaowawezesha kuendelea kupata huduma.
Kwa wananchi wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji, Mwakisale amesema DUWASA itawafikia katika maeneo yao na kurahisisha mchakato wa kupata huduma hiyo.
Amesema mteja anayehitaji kuunganishiwa maji anatakiwa kuwa na kitambulisho pamoja na picha moja, ambapo DUWASA inaweza kumsajili na kumpatia namba ya akaunti kwa ajili ya kuendelea na taratibu za malipo na hatimaye kuunganishiwa huduma.
Mwakisale amesema Wiki ya Huduma kwa Mteja itakuwa fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za DUWASA kwa urahisi, huku changamoto na malalamiko yao yakishughulikiwa kwa wakati.
“Wiki hii itakuwa ni wiki ya faida sana kwa wateja wetu, hasa ambao wanahitaji huduma zetu za DUWASA kwa karibu nao. Lakini pia kwa wote wenye matatizo, tutayatatua kwa urahisi na katika ule wakati wa haraka zaidi,” amesema.
Amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kuwasilisha malalamiko, mahitaji na changamoto zao kwa DUWASA, akisisitiza kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji ya wateja.









No comments:
Post a Comment