
NA SHUA NDEREKA, OKULY Blog, MOROGORO
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), umekamilisha uchaguzi wa Bodi ya Wakurugenzi, huku Mendrack Shem Nziku akichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa mtandao huo.
Nziku anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Apollo Chamwela, ambaye amemaliza kipindi chake cha uongozi baada ya kuitumikia MVIWATA kwa miaka sita.
Uchaguzi huo umefanyika mkoani Morogoro, katika Mkutano mkuu wa 31 wa MVIWATA, ambapo umewakutanisha wanachama kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambao walipiga kura kuwachagua viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi watakaosimamia mtandao huo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Kabla ya uchaguzi huo, Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Stephen Ruvuga, aliwakumbusha wanachama kuhusu utaratibu wa uchaguzi kwa mujibu wa Katiba na kanuni ya mtandao huo.
Alisema Bodi ya Wakurugenzi inaundwa na Mwenyekiti, Mweka Hazina pamoja na wajumbe saba wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu, huku Mkurugenzi Mtendaji akiwa mjumbe wa Bodi kwa nafasi yake, akihudumu kama Katibu wa Bodi.
“Katika Ibara ya 17 ya Katiba ya Mtandao wa Vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) inaeleza kuwa, viongozi isipokuwa Mkurugenzi Mtendaji, watachaguliwa na Mkutano mkuu kwa muhula wa miaka mitatu, na wanaweza kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine na mwisho wa miaka mitatu”. Alisema Ruvuga
Alisema kanda tatu ziliwasilisha majina ya wagombea, ikiwemo Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na Pwani, iliyowasilisha wagombea wa nafasi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, akiwemo Daniel Wilson kutoka Tanga na Odilia Jovin kutoka Morogoro.
Kanda ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ilimtoa mgombea mmoja, Noel Chizua, huku Kanda ya Mara, Mwanza na Simiyu ikiwasilisha wagombea wawili, Alfonce Kulwa kutoka Mara na Sophia Lugembe kutoka Simiyu.
“Kanda ya Mashariki Odilia Jovin aliibuka mshindi kwa kura 321 na mgombea mwenzake Daniel Wilson akipata kura 157, Alfonce Kulwa kutoka mkoani Mara alipata kura 217 na Sophia Lugembe kutoka Simiyu kura 277 na Jumla ya kura tano ziliharibika kufuatia uchaguzi huo.”
Aidha baada ya kusoma matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa Bodi, Katibu wa Bodi hiyo Stephen Ruvuga, alitangaza jina la Mendrack Shem Nziku kuwa Mwenyekiti mpya wa MVIWATA Taifa na Odilia Jovin kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Ruvuga pia amewashukuru wanachama kwa kushiriki uchaguzi huo kwa utulivu, huku akiwataka kuendelea kuilinda MVIWATA kwa wivu mkubwa na kuhakikisha umoja, mshikamano vinaendelea kuwa msingi wa utendaji wa taasisi hiyo.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi, Mwenyekiti mpya wa MVIWATA Taifa Mendrack Nziku, amewashukuru wanachama kwa imani waliyompa na kuwataka kuendelea kuwa na Upendo, Umoja na Mshikamano katika kuimarisha mtandao huo.
Baadhi ya wanachama wa MVIWATA walioshiriki uchaguzi huo wamepongeza mwenendo wa uchaguzi, wakisema umefanyika kwa haki na utulivu.
Matola Paschal, mkulima kutoka Chanzulu, Wilaya ya Kilosa, alisema wako tayari kuwapa ushirikiano viongozi hao waliochaguliwa ili kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wakulima, taasisi hiyo na taifa kwa ujumla.
“Sisi kama wanawake tutawaunga mkono viongozi, lakini tunaomba waendelee kutupambania wanawake katika changamoto zetu za ukatili, masuala ya ardhi na wote wenye mahitaji maalum. Hususani kupitia MVIWATA, sauti zetu zisikike,” alisema Mariam Joseph, mkulima kutoka Kongwa, Dodoma.
Mendrack Nziku ni mkulima kutoka Kijiji cha Ng’anda, Kata ya Makoga, Wilaya ya Wang’ing’ombe mkoani Njombe na ni mwanachama wa muda mrefu wa MVIWATA ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya mtandao huo.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, Nziku alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kwa kipindi cha miaka mitatu na kiongozi wa ngazi mbalimbali za taasisi, ikiwamo Mwenyekiti wa mikoa ya Njombe, Iringa, Songwe na Mbeya kupitia mtandao huo.
Mratibu wa MVIWATA kutoka mkoa wa Njombe, Innocent Hiluka, anaeleza zaidi kuhusu historia ya uongozi na uzoefu wa Mwenyekiti mpya ndani ya mtandao huo, ambaye amekuwa kiungo kikubwa katika uongozi wake katika mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini.
“Mchango wa Mwenyekiti huyu mpya ni mkubwa sana katika ukuaji wa taasisi. Amekuwa akitumia muda wake kutoa hamasa, kuanzisha mitandao mbalimbali na elimu ya uuzaji mazao kwa pamoja. Hivyo, kuchaguliwa kwake ni imani ya wanachama kwamba anaweza kuiongoza MVIWATA,” alisema Hiluka.
Mendrack Shem Nziku sasa anaiongoza MVIWATA kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2026 hadi 2029, akiwa na majukumu ya kupanga na kusimamia utekelezaji wa shughuli za shirika kulingana na sera, mpango mkakati na miongozo ya shirika kwa mujibu wa Katiba ya mtandao huo, Ibara ya 19.







No comments:
Post a Comment