
Na, Veronica Mwafisi - Moshi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka vijana wanaofanya mafunzo ya awali ya Uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa mstari wa mbele kulinda heshima ya chombo hicho nyeti na hatimaye watakapotoka hapo wawe tayari kulitumikia Taifa katika misingi ya maadili na uzalendo.
Mhe. Kikwete amesema hayo leo tarehe 8 Oktoba, 2026 wakati akifungua mafunzo ya awali ya Uchunguzi kwa vijana hao yanayofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania-Moshi.
“Tambueni kwamba, TAKUKURU ni chombo nyeti sana na cha kiuchunguzi kinachosimamia maadili, hivyo mna wajibu wa kuhakikisha mnakuwa mstari wa mbele kulinda heshima yake, amesisitiza.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa Mafunzo hayo ya awali ya Uchunguzi katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa Uadilifu na Ueledi Mkubwa. Hivyo ni matarajio yangu na ya Serikali kwa ujumla kuwa, mtatilia maanani na kwa uzito unaotakiwa mafunzo haya, ili mkitoka hapa mkawe mabalozi wema wa TAKUKURU katika vituo mtakavyopangiwa kwenda kufanya kazi ameongeza.
Amewasisitiza kufuata miongozo, maelekezo pamoja na taratibu zote zitakazotolewa wakati wote watakapokuwa katika mafunzo pamoja na kuzingatia kila wanachofundishwa kwa umakini mkubwa kwakuwa ndicho kitakachoamua hatma ya ajira ya kila mmoja wao ndani ya TAKUKURU.
Waziri Kikwete amewapongeza vijana hao kwa kufanikiwa kuitwa katika hatua hiyo ya mwisho ya Mchakato wa Ajira wa Taasisi kwani ushindani ulikuwa ni mkubwa sana.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila akiwasilisha taarifa ya utendaji wa TAKUKURU alisema mafunzo hayo ni sharti la kimuundo, hivyo kila anayeajiriwa TAKUKURU ni lazima ashiriki kwani yanawasaidia kupata ujuzi na utalaam wa kuzuia na kupambana na rushwa.
Amesema mafunzo hayo yalianza tarehe 19 Septemba 2026 na yatafanyika kwa muda wa miezi mitano ambapo yataendeshwa kwa njia ya vitendo na nadharia ikiwemo kufundishwa suala la maadili katika Utumishi wa Umma na ajira itatolewa baada ya kuhitimu na kufaulu mitihani itakayotolewa wakati wa mafunzo.














No comments:
Post a Comment