MTAHABWA: WATOTO WAFUNDISHWE KUSOMA ULIMWENGU NA VITABU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 20, 2026

MTAHABWA: WATOTO WAFUNDISHWE KUSOMA ULIMWENGU NA VITABU


“Tunaposema vitabu na usomaji, ni vizuri tuanze na jambo moja muhimu sana katika maisha ya mwanadamu; kusoma ulimwengu kisha kusoma neno,”

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Elimu Dkt. Mtahabwa Oktoba 20,2026 katika viwanja vya Bodi ya Huduma za Maktaba Posta jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba na Tamasha la Vitabu na Usomaji.

Amesema watoto wanapaswa kuanza kujifunza mazingira yanayowazunguka kabla na sambamba na kujifunza kusoma na kuandika, kwa kuwa hatua hiyo huwasaidia kuwafahamu watu, vitu, shughuli na tamaduni zinazowazunguka.

Akifafanua, Dkt. Mtahabwa ametumia dhana ya mwanafalsafa wa Brazil, Paulo Freire, ya “kusoma ulimwengu na kusoma neno”, akisema mtoto anapouelewa ulimwengu wake hujengewa msingi mzuri wa kuelewa zaidi kile anachosoma kwenye vitabu.

Amesema mazingira ya elimu ya awali yanapaswa kuandaliwa kwa namna inayowasaidia watoto kujifunza kupitia vitu halisi, watu na mazingira yao, huku wakihamasishwa pia kusoma vitabu vilivyo katika nakala ngumu na nakala laini.

“Tuwa­fundishe watoto kusoma vitabu sana, na tuanze kwa kuwafundisha kusoma ulimwengu,” amesema Dkt. Mtahabwa, akisisitiza kuwa uwezo wa kusoma ulimwengu na vitabu humsaidia mtoto kuwa mtu aliyeelimika na mwenye uwezo wa kuelewa na kukabiliana na maisha kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment