
NA SHUA NDEREKA, OKULY BLOG, MOROGORO
Jumla ya wakulima 58,916 nchini wamefikiwa na kunufaika na shughuli mbalimbali zilizotekelezwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kati ya Januari na Desemba 2025, sawa na asilimia 90 ya wakulima 65,000 waliolengwa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2025 katika Mkutano Mkuu wa 31 wa MVIWATA unaofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo, Stephen Ruvuga, alisema shughuli hizo zililenga kuwawezesha wakulima na vijana kuboresha huduma za kijamii na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya maeneo yao.
Ruvuga alisema miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 imetekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, baada ya wakulima kuibua mahitaji ya maendeleo katika vijiji vyao na kuyafuatilia hadi kujumuishwa kwenye mipango na bajeti za halmashauri.
Alisema kati ya miradi hiyo ni sita ya miundombinu yenye thamani ya shilingi milioni 194.9, ikiwemo ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Lupeta, mradi wa maji Inzomvu, pamoja na ujenzi wa barabara na zahanati katika Kijiji cha Idaho.
Miradi mingine ni ujenzi wa vyoo katika Kijiji cha Mungui na jengo la kujifungulia katika Kijiji cha Ikuyu, ambayo kwa pamoja inakadiriwa kuwahudumia wananchi 22,431.
Katika wilaya za Chamwino, Kongwa na Bahi mkoani Dodoma, Ruvuga alisema wakulima waliibua miradi 13 ya maendeleo kama vipaumbele vyao, ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, ofisi za vijiji na ukamilishaji wa nyumba za watumishi wa afya ambapo miradi hiyo ilijumuishwa katika mipango ya maendeleo ya wilaya.
Aidha, MVIWATA ilitoa mafunzo kwa washiriki 426, yakilenga kuwawezesha wakulima kuongeza uwajibikaji katika matumizi na usimamizi wa rasilimali za umma, kati yao wakulima walikuwa 154 na viongozi wa serikali 272.
“Mada kuu zilikuwa mbinu za mipango ya fursa na vikwazo vya maendeleo, mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma pamoja na mikakati ya kuimarisha mitandao ya wakulima ili kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya taifa,” alisema Ruvuga.
Katika kuimarisha mshikamano wa wakulima wadogo kitaifa, kikanda na kimataifa, MVIWATA kwa kushirikiana na International Association for Popular Cooperation iliandaa mafunzo ya kilimo ikolojia yaliyowakutanisha washiriki 32 kutoka Kenya, Ghana, Liberia, Cameroon, Morocco, Palestina, Brazil, Argentina na Tanzania.
Pia alisema wakulima vijana 48 kutoka nchi 20 za Ulaya, Asia, Afrika na Amerika walishiriki katika mafunzo na majadiliano kuhusu mustakabali wa wakulima katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni uhuru wa chakula, mbinu za kilimo ikolojia na changamoto ya uporaji wa ardhi.
“Kongamano hili lilihusisha ziara katika Tarafa ya Mgeta kwa lengo la kujifunza hali halisi ya maisha ya mkulima wa Tanzania, kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kilimo ikolojia na kupanda miche 50 ya parachichi katika bustani ya shule,” alisema Ruvuga.
Michael Kobelo, mkulima kutoka Tarafa ya Mgeta mkoani Morogoro, alisema baada ya kupata mafunzo ya kilimo ikolojia kutoka MVIWATA, wameanza kutumia mbolea za asili katika uzalishaji kwa lengo la kulinda usalama wa wazalishaji na walaji na kupunguza matumizi ya kemikali shambani.
Sambamba na hayo, MVIWATA iliwezesha uanzishwaji wa Klabu za Kilimo na Mazingira katika shule 28 za mikoa ya Ruvuma, Manyara, Njombe, Kilimanjaro na Morogoro, ambapo wanafunzi 969 walishiriki.
Kupitia klabu hizo, wanafunzi walijifunza kwa vitendo mbinu za kilimo ikolojia, uhifadhi wa mazingira, uzalishaji wa mboga na utayarishaji wa pembejeo za asili.
Mratibu wa Mtandao wa Vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani Njombe Innocent Hiluka alisema, lengo la kuanzisha Klabu za Kilimo na Mazingira katika shule hizo ni kutoa uelewa na kuwajengea msingi wa utunzaji wa mazingira ili kuwa mabalozi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kurithisha kilimo endelevu kwa vijana
Akizungumzia mafanikio ya Klabu ya Kilimo na Mazingira kutoka shule ya Sekondari Ninga mkoani Njombe, Mwalimu mlezi wa Klabu hiyo Boniphace alisema, kupitia mafunzo yaliyotolewa na MVIWATA, wamefanikiwa kuzalisha mahindi, parachichi, miti ya mbao na mbogamboga.
“Kwa kuwa wanafunzi wanaishi shuleni, hali hii ilituhamasisha kuzalisha mboga mboga na matunda ili kuboresha afya na lishe yao, katika uzalishaji huo wa mbogamboga tunatumia samadi kama mbolea, ambayo wanafunzi huleta kutoka nyumbani, kwa kuwa shule yetu ipo karibu na makazi ya watu ambapo imesaidia kuboresha ukuaji wa mazao kupitia Klabu ya Mazingira,” alisema Mwalimu Boniphace.
“Hapo awali tulikuwa tukila maharage bila mboga za majani, klabu yetu imechangia sisi wananfunzi kula mboga za majani kila siku na tunaporudi nyumbani wakati wa likizo baada ya shule kufungwa, tunaendelea kutumia ujuzi tulioupata kwa kutengeneza bustani ili kusaidia familia zetu kupata mboga na kipato baada ya mauzo,” alisema Selina Joseph, mwanafunzi wa shule hiyo na Katibu wa Klabu ya Mazingira.
MVIWATA imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa wakulima wadogo kutokana na mchango wao katika uchumi na uzalishaji wa chakula nchini na duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2025, juhudi hizo zimechangia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wakulima wadogo, ikiwemo elimu, barabara, afya, maji na nishati.


Good work
ReplyDelete