REA, BENKI YA DUNIA WAPELEKA TABASAMU KWA WANANCHI WAISHIO VISIWANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 24, 2026

REA, BENKI YA DUNIA WAPELEKA TABASAMU KWA WANANCHI WAISHIO VISIWANI



Na Mwandishi Wetu - Mwanza


Wananchi wanaoishi katika Visiwa wameipongeza na kuishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwafikishia mifumo ya umeme jua kwa bei ya ruzuku hali iliyosaidia kuboresha maisha yao visiwani.

Pongezi hizo zimetolewa leo na wananchi wanaoishi katika Kisiwa cha Bezi kilichopo katika Wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ilipotembelea kisiwani hapo kuona maendeleo ya mradi huo ambao unafadhiliwa na benki hiyo na kusimamiwa na REA katika visiwa 120 nchini.

“Awali tulikuwa tunapata changamoto sana ya nishati ya umeme. Ilikuwa ikifika usiku, giza lilikuwa linatanda katika kisiwa chetu. Lakini tangu REA ianze kutekeleza mradi huu kumekuwa na mabadiliko makubwa sana. Kumekuwa na mwanga, wananchi wanaweza kuchaji simu zao tofauti na hapo awali ambapo tulikuwa tunalazimika kulipia sehemu maalum ambazo wanachajisha simu ili kupata huduma hiyo,” amesema Bi. Chiju Ramadhan ambaye ni mkazi wa kisiwani hapo.

“Kwa kweli manufaa ni makubwa sana ya huu mradi tangu umeingia hapa kisiwani. Lakini tulikuwa tunaomba tupatiwe mifumo mikubwa zaidi yenye uwezo wa kuwasha mafriji kwa ajili ya kuuza vinywaji baridi lakini pia kugandisha samaki. Shughuli kubwa ya hapa kisiwani ni uvuvi, hivyo tukipata mifumo yenye uwezo mkubwa zaidi tutaweza kugandisha samaki na kuuza muda wote, tofauti na hivi sasa ambapo tunalazimika kusafirisha kwenda kuwahifadhi mjini,” amesema Pascal Patrick ambaye ni mkazi wa kisiwani hapo.

Awali akitoa taarifa kuhusu utekelezwaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini na umelenga kuwanufaisha wananchi wanaoishi katika Visiwa 120 huku ukigharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 8.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mwijage, mradi huo unatekelezwa kwa njia ya ruzuku ambapo serikali imetoa ruzuku kuanzia asilimia 55 mpaka asilimia 75 katika mifumo hiyo ya umeme jua na wananchi wakichangia asilimia zilizobaki kutegemeana na ukubwa wa mfumo.

“Hizi zote ni juhudi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Wabia mbalimbali wa Maendeleo wakiwamo Benki ya Dunia kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati ya umeme kwa maendeleo endelevu,” amesema Mhandisi Mwijage.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ambaye pia ni Mtaalam wa Nishati kutoka Benki hiyo, Dkt. Rhonda Jordan amepongeza utekelezwaji wa mradi huo huku akisema kuwa wameshuhudia ni kwa namna gani mradi huo umeweza kuwa chachu ya kubadilisha maisha ya wananchi katika kisiwa hicho.








No comments:

Post a Comment