BMH YATOA WITO KWA JAMII KUWALETA WATOTO WENYE MATATIZO YA MIGUU KIFUNDO KUJA KUPATA MATIBABU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 28, 2026

BMH YATOA WITO KWA JAMII KUWALETA WATOTO WENYE MATATIZO YA MIGUU KIFUNDO KUJA KUPATA MATIBABU



Na Gladys Lukindo, Jeremia Mwakyoma, Godfrey Mwiliko
- DODOMA


Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetoa wito kwa jamii kuhakikisha inawaleta hospitalini hapo, watoto wote wenye matatizo ya miguu kifundo kuja kupata matibabu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Fiziotherapia wa BMH Hubert Mtalo wakati wa kambi ya matibabu kwa watoto wenye matatizo hayo ambapo ametumia nafasi hiyo kuihakikishia jamii kuwa tatizo hilo linatibika.

"Napenda kuiasa jamii isiwafiche watoto wenye matatizo ya miguu kifundo kwa kuwa ni tatizo la kawaida na linatibika, hivyo wawalete hospitalini haraka mara tu wanapowagundua bila kuwachelewesha, hiyo inasaidia kufanya matibabu yao kuwa rahisi" alisisitiza Mtalo.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuishukuru Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (BMF) kwa kufadhili gharama za matibabu hayo ya miguu kifundo kwa Watoto.

"Tunaishukuru Taasisi ya BMF kwa kufadhili gharama za matibabu haya kwa watoto hapa hospitalini, hiyo imewezesha watoto wenye tatizo la miguu kifundo kutibiwa bure bila malipo, hivyo naomba wazazi na walezi wawalete watoto waje kupata matibabu" alisisitiza Mtalo.

Kwa upande wake Mtaalamu wa matibabu ya Fiziotherapia wa BMH George Kennedy amefafanua kuwa mtoto kuzaliwa na tatizo la miguu kifundo linasababishwa na mtoto kukaa vibaya akiwa tumboni wakati wa ujauzito na miguu kujikunja kwenye kifundo kwa aina hiyo, na baadhi chanzo kamili hakifamiki lakini pia watoto wenye shida ya kichwa kikubwa kilichojaa maji na mgongo wazi inachangia kupata tatizo hilo wakati watoto wengine wanarithi kutoka kwa wazazi.

Nae Mtaalamu wa Fiziotherapia Charles Nyangusi amesema kuwa matibabu hayo hadi kukamilika kwake yanachukua muda wa miaka minne hadi minne na nusu na mtoto apona kabisa miguu yake inakaa vizuri.

Kwa upande wake Bi. Rebecca Joseph kutoka Mkoani Singida ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye changamoto ya miguu kifundo, ameshukuru kwa mtoto wake kupatiwa matibabu sahihi, hali yake inazidi kuimarika na ametoa wito kwa jamii kuacha mtazamo mbaya wa kuwatenga watoto wenye changamoto hizo na wazazi wao badala yake wawe nao pamoja, kuwasaidia, kushirikiana nao na kuwatia moyo.





No comments:

Post a Comment