
Na. Okuly Julius- OKULY BLOG,DODOMA
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka Watanzania kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati na kupunguza gharama za matibabu kwa familia na Serikali.
Dkt. Samizi ametoa wito huo Novemba 29,2026 wakati wa NHIF Marathon 2026 iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambapo amesisitiza umuhimu wa wananchi kujenga utamaduni wa kujikinga na magonjwa badala ya kusubiri kuugua.
Amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kujenga Tanzania yenye afya njema kwa kuwekeza zaidi katika kinga dhidi ya magonjwa, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za matibabu na kuelekeza rasilimali katika shughuli za maendeleo.
Akizungumzia kampeni ya Zijue Namba Zako iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Mohamed Omari Mchengerwa, amesema wananchi wanapaswa kufahamu viashiria muhimu vya afya zao, ikiwemo shinikizo la damu, sukari na mafuta mwilini pamoja na afya ya figo ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema asilimia 61 ya mapato ya NHIF yanatumika kuhudumia wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, akiwataka wananchi kufanya mazoezi, kula chakula bora, kupunguza matumizi ya pombe, kuepuka uvutaji sigara na kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka.
Kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, Dkt. Samizi amesema katika awamu ya kwanza Serikali ililipia kaya 276,000 zisizo na uwezo kwa gharama ya Shilingi bilioni 48, huku asilimia 90 ya kaya hizo zikiwa zimeanza kunufaika na huduma za afya, hususan katika vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi.
Ameeleza kuwa katika awamu ya pili iliyozinduliwa Oktoba 22, 2026, mkoani Mtwara, Serikali inalenga kusajili kaya nyingine 625,000 ili kufikisha kaya 901,000 zitakazolipiwa na Serikali, kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 98.
Aidha, amewahimiza wananchi wenye uwezo kujiunga na mpango huo kupitia kifurushi cha Bahari cha Shilingi 150,000 kwa mwaka, kinachotoa huduma 370 za afya kwa kaya yenye watu sita, sawa na Shilingi 25,000 kwa kila mtu kwa mwaka, akisisitiza kuwa bima hiyo inaweza kuwa zawadi muhimu kwa familia katika kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Dkt. Samizi amempongeza Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kwa juhudi za kusimamia sekta ya afya na kuhimiza utekelezaji wa maono ya Rais Samia, akibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa usawa.

No comments:
Post a Comment