
Na Okuly Julius, OKULY BLOG – DODOMA
Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amewaagiza watendaji na wataalamu wa sekta ya afya nchini kuhakikisha kila Mtanzania anayefika katika kituo cha kutolea huduma za afya anahamasishwa kujiunga na bima ya afya ili kujihakikishia upatikanaji wa matibabu wakati wowote anapohitaji huduma.
Aidha, amewataka Watanzania kuzingatia utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kupima afya zao ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaendelea kuongeza mzigo wa gharama za matibabu nchini.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Novemba 29, 2026, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wakati wa mbio za NHIF Marathon 2026 zilizofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Amesema ushiriki wa takribani watu 10,000 katika mbio hizo ni ishara ya kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga afya bora kupitia mazoezi na mtindo bora wa maisha.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za bima ya afya, Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mifumo ya huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bila kikwazo cha kukosa fedha taslimu, ikiwemo kutenga takribani shilingi bilioni 98 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wasio na uwezo.
Ameeleza kuwa NHIF imezindua kifurushi cha bima ya afya ya kaya cha shilingi 105,000 kwa mwaka, kinachomjumuisha mwanachama, mwenza wake na wategemezi wanne, hatua inayowezesha familia kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.
Amesema kifurushi hicho kinatoa fursa ya kupata huduma katika ngazi mbalimbali za vituo vya afya, zahanati, hospitali za halmashauri na mikoa hadi hospitali za rufaa, kanda na taifa.
Katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga na bima ya afya, Mchengerwa amezitaka hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini, vinavyokadiriwa kufikia zaidi ya 12,000, kuimarisha utoaji wa elimu ya bima kwa kila mgonjwa anayefika kupata huduma.
Amesisitiza kuwa wahudumu wanapaswa kumpokea mgonjwa kwa heshima, kumsikiliza na kumpatia huduma bora bila ubaguzi, kisha kumwelekeza kuhusu umuhimu na faida za kuwa na bima ya afya.
Aidha, amewataka wataalamu wa afya kuuliza wagonjwa au watu wanaowasindikiza iwapo wana vitambulisho vya bima ya afya baada ya hatua za awali za kitaalamu, na kwa wale ambao hawana, wawaeleze gharama za matibabu pamoja na faida za kujiunga na bima.
Sambamba na hilo, amemtaka Mkurugenzi wa NHIF na wasaidizi wake kuboresha mifumo ya kidijitali ili kuondoa ucheleweshaji wa utoaji wa vitambulisho vya bima na kuhakikisha watoa huduma za afya wanalipwa madai yao kwa wakati.
Amesema Serikali imeendelea kupunguza muda wa malipo ya madai kutoka siku 120 hadi siku 45 ili kuimarisha ufanisi wa huduma na kuongeza imani ya wadau kwa mfuko huo.
Katika hatua nyingine, akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mchengerwa amesema afya bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanachukua zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya jumla ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mameneja wa maeneo mbalimbali nchini kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kupima afya zao na kufuatilia uzito pamoja na ukubwa wa kiuno ili kujikinga na magonjwa ya moyo, kisukari, saratani na magonjwa ya figo.
“Taifa lisilo na watu wenye afya njema ni sawa na taifa mfu. Tuamke asubuhi tufanye mazoezi, tukirejea jioni tufanye mazoezi, tupime afya zetu na tujilinde ili taifa letu liweze kusonga mbele,” amesema Mchengerwa.
Vilevile, amewapongeza viongozi, wabunge na wananchi waliojitokeza kushiriki mbio hizo, akiwemo Lusinde aliyeshiriki mbio za kilomita 25, huku akiwataka Watanzania kuendeleza utamaduni wa mazoezi kama sehemu ya kujenga jamii yenye afya bora.
Maadhimisho hayo ya miaka 25 ya NHIF yanaendelea kuwa sehemu ya kutathmini mchango wa mfuko huo katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya na kuimarisha ustawi wa wananchi nchini.










No comments:
Post a Comment