QWARAY: WATUMISHI WA UMMA WARUDISHE TABASAMU LA WANANCHI KWA UADILIFU NA UWAJIBIKAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 26, 2026

QWARAY: WATUMISHI WA UMMA WARUDISHE TABASAMU LA WANANCHI KWA UADILIFU NA UWAJIBIKAJI




Na Okuly Julius, OKULY BLOG – DODOMA


Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, amewataka watumishi wa umma na taasisi zinazosimamia maadili kuongeza uwajibikaji, uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kurejesha imani ya wananchi kwa serikali na kuboresha utoaji wa huduma za umma.

Qwaray amesema kurejea kwa tabasamu la wananchi, kama alivyowahi kusisitiza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kunategemea kwa kiasi kikubwa namna watumishi wa umma wanavyotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya maadili, usikivu na uwajibikaji.

Amesema wananchi wanahitaji huduma bora zinazotolewa kwa wakati, bila urasimu, rushwa, lugha zisizo na staha wala upendeleo, akisisitiza kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili.

Naibu Waziri huyo ameyasema hayo, Novemba 26,2026 jijini Dodoma, wakati akifungua Kikao Kazi cha Saba cha Kubadilishana Uzoefu na Kuimarisha Ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – Utumishi, taasisi zinazosimamia maadili ya utendaji na mamlaka zinazosimamia maadili ya kitaaluma, kilicholenga kuimarisha utawala bora na kujenga uwezo wa pamoja katika kusimamia maadili ya utumishi wa umma.

Amesema utaratibu wa vikao hivyo ulioanzishwa mwaka 2018 umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa taasisi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa maadili, huku akizitaka kuweka mkazo zaidi katika kuhamasisha uadilifu na kujenga utamaduni wa uwajibikaji ndani ya taasisi za umma.

Hata hivyo, Qwaray ameeleza kuwa licha ya serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi na utoaji wa huduma, bado zipo taarifa za viashiria vya ukiukwaji wa maadili, ikiwemo rushwa, uvujishaji wa siri za serikali, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, hujuma dhidi ya miradi ya maendeleo pamoja na upungufu wa uzalendo.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inahitaji usimamizi madhubuti wa maadili na uwajibikaji wa kila mtumishi, kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hususan Ibara ya 8(1)(b) na 35(1), ili kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa chombo cha kuwatumikia wananchi kwa haki na uadilifu.

Aidha, amezitaka taasisi simamizi za maadili kuimarisha mifumo rafiki ya kupokea na kushughulikia maoni na malalamiko ya wananchi, kuhakikisha miongozo na nyaraka za maadili zinapatikana kupitia tovuti rasmi, pamoja na kufanya tathmini na tafiti za mara kwa mara ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Amesisitiza kuwa kuimarika kwa maadili, uwajibikaji na usikivu katika utumishi wa umma ni msingi muhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa serikali, kuboresha huduma na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Leila Mavika, amesema taasisi na mamlaka zinazosimamia maadili zinapaswa kuongeza usikivu, uwazi na uwajibikaji ili kujenga utamaduni wa uadilifu na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali.

Mavika amesema kikao hicho cha siku mbili ni jukwaa muhimu la kubadilishana taarifa, uzoefu na maarifa kati ya taasisi zinazohusika na usimamizi wa maadili, pamoja na kujengeana uwezo kuhusu namna bora ya kusimamia maadili ya kisekta na kuboresha huduma zinazowafikia wananchi moja kwa moja.

Amebainisha kuwa taasisi hizo zina wajibu wa kusimamia misingi ya sheria, uwazi, uwajibikaji, haki na usawa, sambamba na kupinga vitendo vya rushwa na ukiukwaji mwingine wa maadili unaoweza kuathiri maslahi ya umma.

Ameongeza kuwa washiriki wa kikao hicho wanapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa wizara na taasisi mbalimbali, zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Afya pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kwa mujibu wa Mavika, ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha changamoto za kimaadili zinazojitokeza katika sekta mbalimbali zinapatiwa ufumbuzi na kwamba uwajibikaji unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila taasisi ya umma.






No comments:

Post a Comment