Tanzania na Nigeria zimeungana kuandaa Mkutano wa Kwanza wa Afya ya Wanawake Afrika (Women’s Health Africa Summit 2026), utakaofanyika Desemba 1, 2026, jijini Abuja, Nigeria, kwa lengo la kuimarisha uwekezaji, rasilimali watu katika sekta ya afya na huduma za afya zinazotolewa katika jamii. Akizungumza jijini Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa uzinduzi wa Mpango Kazi wake kama Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inafurahi kushirikiana na Nigeria kuandaa mkutano huo, akieleza kuwa nafasi za Kinara wa Umoja wa Afrika za nchi hizo mbili zinakamilishana katika kuendeleza afya ya wanawake.
“Mkutano huo utalenga kuimarisha ufuatiliaji wa kisiasa na uwajibikaji katika kutekeleza ahadi za kufikia malengo ya Sifuri Tatu (Three Zeros), sambamba na kuendeleza nguvu kazi ya sekta ya afya na huduma za afya zinazotolewa katika ngazi ya jamii” alisema Rais Samia
Kwa upande wake, Rais wa Nigeria, Mhe. Bola Ahmed Tinubu, ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Rasilimali Watu katika Afya na Ushirikiano wa Utoaji wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, anaunga mkono ajenda ya kuimarisha nguvu kazi ya afya na utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu “Health Workforce for Better Women’s Health”, ukiwakutanisha viongozi wa Serikali, Mawaziri wa Afya, wataalamu na washirika wa maendeleo kujadili uwekezaji na mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wanawake na wasichana barani Afrika.
Kupitia mkutano huo, Tanzania na Nigeria zinalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuharakisha hatua za kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma bora za afya, huku juhudi za kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa mama na mtoto zikiendelea kupewa kipaumbele.

No comments:
Post a Comment