TGNP YAPAZA SAUTI DHIDI YA UPORAJI NA DHULUMA WA MALI ZA MIRATHI KWA WAJANE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 25, 2026

TGNP YAPAZA SAUTI DHIDI YA UPORAJI NA DHULUMA WA MALI ZA MIRATHI KWA WAJANE

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umehimiza jamii kuachana na mila na desturi zinazowanyima wajane haki ya kumiliki na kurithi mali zilizoachwa na wenza wao, huku ukitaka sheria za mirathi nchini kufanyiwa mapitio ili kuendana na mazingira ya sasa ya kijamii na kiuchumi.

Wito huo umetolewa leo Novemba 25, 2026 Jijini Dar es Salaam katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zilizofanyika kupitia TGNP, zilizojadili mada isemayo “Uporaji wa Mali za Mirathi na Dhuluma ya Kiuchumi Dhidi ya Wajane: Je, Sheria na Jamii Zinamtendea Haki Mwanamke Aliyefiwa na Mwenza?”

Akichambua mada hiyo, Mwanasheria na Mwezeshaji wa mada hiyo, Lameck Wilson, amesema uchambuzi wa sheria na hali halisi ya kijamii umebaini kuwa wajane wengi wanakabiliwa na changamoto za kunyimwa haki ya kumiliki mali za mirathi, hasa pale wanapokutana na upinzani kutoka kwa ndugu wa marehemu.

Amesema sheria zinazohusika na usimamizi na ugawaji wa mirathi nchini ni pamoja na Probate and Administration of Estates Act, Indian Succession Act, sheria za Kiislamu na sheria za kimila, ambazo hutumika kutegemea mazingira na utaratibu wa marehemu.

Hata hivyo, amesema baadhi ya sheria za kimila na desturi za jamii bado zinachangia kuwanyima wanawake haki ya kumiliki mali, hususan ardhi, licha ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutambua haki ya kila mtu kumiliki mali.

Wilson amesema changamoto nyingine inajitokeza katika familia ambazo marehemu alikuwa na wake zaidi ya mmoja, ambako kutokuwepo kwa mwongozo unaoeleweka kwa baadhi ya mazingira ya ugawaji wa mali kunaweza kuongeza migogoro na kuwaweka wajane katika mazingira magumu.

Ameongeza kuwa kifo cha mwenza kinaweza kusababisha mjane kupoteza vyanzo vya kipato na mahitaji aliyokuwa akiyapata kupitia marehemu, yakiwemo chakula, bima ya afya na msaada wa kifedha, huku akiendelea kutumia muda na rasilimali kufuatilia haki yake ya mirathi.

Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya sheria za mirathi kwa wanawake na jamii kwa ujumla, pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa dini ili waweze kusaidia wanandoa na familia kutatua changamoto hizo kabla hazijawa kubwa.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa kupitia upya sheria zinazotumika katika masuala ya mirathi, akitolea mfano Indian Succession Act ya mwaka 1865, akieleza kuwa ni muhimu kuwa na sheria zinazoendana na mazingira, mahitaji na hali ya uchumi wa Tanzania wa sasa.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijichi, Dar es Salaam, Magreth Matongo Mwita, amesema baadhi ya jamii bado zinamchukulia mwanamke kama mtu asiye na haki ya kumiliki mali za familia, hali inayosababisha wajane kufukuzwa katika nyumba na kunyang'anywa mali na ndugu wa marehemu.

Amesema hali hiyo inakiuka mchango wa mwanamke katika kujenga familia na kuchuma mali akiwa pamoja na mumewe, akisisitiza kuwa ni muhimu jamii kutambua mchango huo na kumpatia mjane haki yake.

Naye mdau wa Semina za Jinsia na Maendeleo, Kennedy Angelita, amesema utegemezi wa kiuchumi kwa waume, kutofahamu sheria za mirathi na hofu ya migogoro na ndugu wa marehemu ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wajane wengi kushindwa kudai haki zao.

Amesema baadhi ya wajane huogopa kufungua mashauri ya mirathi wakihofia gharama na uhasama wa kifamilia, huku wengine wakiamua kuacha kufuatilia mali hizo na kujikita katika kulea watoto wao.

Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuelewa kuwa mirathi ni haki ya mjane na ni sehemu muhimu ya ustawi wa familia, kwani mwanamke anapopata haki yake ya msingi, watoto pia wananufaika kupitia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo elimu na malezi bora.

No comments:

Post a Comment