Tume ya Vyuo vikuu (TCU) imesema katika kuhakiki ubora, imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara,wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa,kikanda na kimataifa.
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof.Charles D. Kihampa leo Februari 22,2023,wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita ,mbele ya waandishi wa habari,Jijini Dodoma.
Amesema kuwa TCU imeweka utaratibu wa kuanzishwa na kuimarishwa mifumo ya uthibiti ubora ndani ya vyuo vikuu ambapo vyuo vyenyewe vimekuwa na utaratibu wa kujikagua,kujitathmini na kufanya marekebisho mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya uendeshaji wa vyuo vikuu.
"kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari ,2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa, na zoezi hili la ukaguzi wa vyuo ni endelevu kila mwaka"amesema Prof.Kihampa
Aidha,Prof. Kihampa amesema katika kuwajengea uwezo wahadhiri na viongozi wa vyuo vikuu hususani utolewaji wa elimu ya chuo kikuu ,TCU imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo kwa viongozi,wahadhiri na maofisa wa vyuo vikuu vya umma na binfsi hapa nchini.
Kihampa amesema kuanzia mwaka wa fedha wa 2022/23 ,serikali imetenga kiasi cha bilioni 6.4 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kichumi kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuishwa kwa kuzingatia maoni ya wadau ili kukidhi matarajio na mahitaji ya soko.
Akizungumzia kuhusu suala la udahili wa wanafunzi , katika shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2022/23 ni 113.383 ukilinganisha na mwaka 2020/21 ambapo ulikuwa ni 87,934 ambapo ongzeko hilo ni sawa na asilimia 28.9 ,ongeko hilo likichagizwa na kuongezeka kwa fursa za masomo ya elimu ya juu na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Katibu Mtendaji huyo amesema kuwa kutokana na kuimarishwa kwa programu za elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Elimu ya Chuo Kikuu, imesaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya TCU na taratibu za uendeshaji wa elimu ya chuo kikuu na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto wanazokutana nazo wanafunzi na wadau wengine wa elimu ya juu katika kipindi cha hivi karibuni ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.


No comments:
Post a Comment