Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali itaendelea kuimarisha Afua mbalimbali zinazolenga kumlinda Mtoto wa kiume dhidi ya Ukatili wa Ulawiti.
Akifungua kongamano la siku moja lililoandaliwa na Taasisi ya Vuka initiative, Mkoani Dodoma Mei 05, 2023, Mhe.Mwanaidi ameeleza kwamba matukio ya ukatili dhidi ya watoto wa kiume yatakwisha iwapo jamii itawajibika katika malezi ya watoto kwa ushirikiano ili kuondokana na wimbi la ulawiti dhidi ya Watoto wa kiume.
“Mtoto wa jirani yako ni wa kwako na popote utapomkuta anafanyiwa vitendo vya ukatili ni jukumu lako kuzuia na endapo unaona viashiria vya mtoto kufanyiwa Ukatili ni wajibu wako kuzuia,hivyo naisihi jamii iwe na ushirikiano katika kulea Watoto” Alisema Mwanaidi.
Lakini pia Naibu Waziri amewasihi wazazi kutenga muda wa kuzungumza na Watoto wao wa kiume kabla hawajaharibika na kupoteza mwelekeo maishani.
“Tumeshuhudia baadhi ya watoto wetu wakijihusisha na mapenzi ya jinsia moja na hii ni hali inayosikitisha,Mtoto wa kiume akishaharibiwa hawezi kusaidiwa tena,Ni matumaini yangu kongamano hili litakuja na ufumbuzi wa maadili ili kutatua changamoto hii” amesema Mhe. Mwanaidi.
Aidha,Mkurugenzi wa Maendeleoa ya Mtoto, Sebastian Kitiku kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii amebainisha kuwa, Serikali kupitia mwongozo wa malezi ambao unasisitiza wazazi kuwapa watoto mahitaji ya msingi lakini pia kumlinda mtoto dhidi ya ukatili kwani sehemu kubwa ya ukatili unafanyika nyumbani.
“Wazazi wengi wamechanganyikiwa na hawafahamu mbinu gani ya kuwalea watoto wao na yote hayo yameletwa na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia pamoja na muungiliano wa mila na desturi hivyo baadhi ya wazazi wanakua wakali kupita kiasi,lakini pia kuna wazazi wanaowaachia watoto kila wanachokitaka hivyo kuwafanya watoto kubweteka na mwisjo wa siku kukua kuwa watu wazima wanaotaka vitu kwa urahisi hatimaye kujikuta wanaijiingiza kwenye vitu visivyofaa”Alisema Kitiku.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Shirika la Vuka initiative Veronica Ignatus amesema Taasisi ya Vuka initiative imeendelea na Kampeni inayojulikana kama”Mlinde mtoto wa kiume dhidi ya ukatili wa Ulawiti” lenye dhumuni la kumkumbusha Mwanamke kumlinda mtoto wa kiume kwani ndiye mlinzi wa Familia wa baadae.
“Lengo ni kuwawezesha wazazi kuzitambua changamoto na kuzitatua ili kumuokoa mtoto wa Kiume dhidi ya katili kwani ukatili huu unatokana na wazazi kutumia muda mwingi kutafuta mali na kushindwa kumsikiliza mtoto wa kiume hivyo kupelekea kumnyima haki yake ya kumsikiliza”Alisema Veronica.
No comments:
Post a Comment