Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali tayari imeshampata Mkandarasi na kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 kwa kiwango cha lami.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongezwa kwa ujenzi wa kilometa 10 katika barabara hiyo ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji kwa kuinganisha na kipande kilichobakia cha Kimbiji hadi Cheka kwa kiwango cha lami.
Bashungwa amezungumza hayo Aprili 29, 2024 Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana na mvua za El-Nino na kujionea hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).
“Nilivyokuja Kigamboni kukagua barabara hii ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji tulikuwa hatujasaini mkataba, nitumia nafasi hii kuwataarifu kuwa tayari tumesaini mkataba na sasa Mkandarasi anaendelea kuleta mitambo eneo la kazi ili mvua itakapokatika aweze kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami na haitakuwa kilometa 41 tena bali 51 kwani tunaiunganisha na kipande kilichobakia cha Cheka hadi Kimbiji”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali iko kazini na imejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TANROADS na TARURA kurekebisha maeneo yote yaliyopata athari ili ziendelee kupitika na kutokwamisha shughuli za wananchi na viwanda katika uzalishaji.
Halikadhalika, Bashungwa amemuelekeza Mkandarasi Estim kuendelea kuleta vifaa na mitambo yote katika eneo la mradi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji wakati akisubiria malipo ya awali na kiangazi kianze ili ujenzi uweze kuanza mara moja.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam hauna mafuriko ila wananchi wameziba njia za maji kwa kujenga nyumba kwenye mikondo ya maji na kusistiza kuwa Mkoa huo unahitaji kufumuliwa upya kwa na kujenga mifereji imara ya maji ya mvua ili kuzuia maji kutoingia kwenye makazi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ameeleza kuwa barabara ya Kibada - Mwasonga hadi Cheka ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Kigamboni kwani inapitisha magari zaidi ya elfu moja ya ujazo mbalimbali makubwa na madogo na pia ni barabara inayoelekea kwenye viwanda vikubwa zaidi ya 10 na kuna eneo kubwa la uwekezaji hivyo ujenzi wa barabara hiyo utaleta tija na chachu ya kimaendeleo kwa wanakigamboni.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. John Mkumbo ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji (km 41) utatekelezwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Estim na tayari ameshakabidhiwa eneo la ujenzi tangu Aprili 10, 2024.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi
No comments:
Post a Comment