Uingereza imetetea uamuzi wake wa kusitisha baadhi ya mauzo ya silaha kwa Israel, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiutaja uamuzi huo kuwa wa "aibu".
Netanyahu alisema kwenye mtandao wa kijamii kwamba uamuzi huo "utawapa ujasiri Hamas." Lakini Husam Zomlot, balozi wa Palestina nchini Uingereza, alielezea marufuku hiyo ya sehemu kama "hatua muhimu ya kwanza kuelekea Uingereza kutimiza majukumu yake ya kisheria chini ya sheria za Uingereza na kimataifa".
Siku ya Jumatatu, Uingereza ilisitisha leseni zipatazo 30 kati ya 350 za kuuza silaha kwa Israel.
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey alisisitiza kuwa Uingereza itasalia kuwa "mshirika mkubwa" wa Israel, akiiambia BBC kwamba usalama wa Israel hautayumbishwa na uamuzi huo.
Mawaziri wa serikali wanasema silaha hizo zinaweza kutumika Gaza kukiuka sheria za kimataifa.
Amnesty International ya Uingereza ilisema hatua hizo ni "finyu sana".
Wengine wamekosoa muda wa kutangazwa kwa mpango huo, ambao uliambatana na siku ya mazishi ya mateka sita waliouawa huko Gaza wiki iliyopita.
"Ilikuwa uchungu sana kuona nyuso za mateka waliokufa," Healy aliiambia BBC, lakini akaongeza kuwa muda wa uamuzi "ulisukumwa na ukweli kwamba huu ni mchakato wa kisheria" huku kukiwa na hitaji la kuarifu bunge.
No comments:
Post a Comment