
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa amesema kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuiwezesha Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kutekeleza huduma zake, ikiwemo Mradi wa Digital Tanzania ambao ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Kadi Jamii.
Kupitia mradi huu, taasisi za umma na binafsi haziitaji tena kuwekeza kwenye mifumo yao binafsi, badala yake zinahimizwa kutumia huduma za NIDC kwa gharama nafuu na kwa usalama wa kuaminika.
Waziri Slaa alieleza hayo baada ziara ya Mhe. Kassim Majaliwa(Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipotembelea Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kwa lengo la kuangalia Mfum wa N- CARD unavyofanya kazi.
Amesema Kadi Jamii, ambayo itaunganishwa na taarifa za NIDA za kila mwananchi, itatumika kufanya miamala mbalimbali ya kifedha na manunuzi, ikiwa ni pamoja na malipo ya viingilio vya viwanja vya michezo, usafiri wa vivuko, UDART na huduma nyingine muhimu.
“Kadi hiyo itarahisisha maisha ya kila siku ya mwananchi kwa kuwa na kadi moja tu ya matumizi mengi, badala ya kubeba kadi nyingi kwa ajili ya huduma tofauti,” alisema.
Ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unafikiwa na wananchi wengi, Waziri Slaa alieleza kuwa Serikali ina mkakati wa kupunguza bei ya simu janja zitakazotumika katika mfumo huo wa kadi.
Aidha, alieleza kuwa hadi sasa Mkongo wa Taifa unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) umeunganisha wilaya 109 kati ya 139, na tayari baadhi ya nchi jirani barani Afrika zimeunganishwa na mkongo huo, hatua itakayosaidia kuimarisha zaidi huduma za kidijitali ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment