ULEGA AUNDA TIMU KUCHUNGUZA KIVUKO CHA MV TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 13, 2025

ULEGA AUNDA TIMU KUCHUNGUZA KIVUKO CHA MV TANGA


Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameunda timu ya wataalamu na kuipa siku saba kuchunguza changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika Kivuko cha MV TANGA kilichopo wilayani Pangani, mkoani Tanga, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa utendaji wake.

Akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani humo, Ulega amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa za ukarabati na ununuzi wa vivuko ili kurahisisha maisha ya wananchi na kwamba wananchi hawapaswi kupata shida wakati miundombinu ipo.

Kivuko ambacho kimeundiwa timu ya uchunguzi kinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni na Ulega alisema lengo ni kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinafanya kazi kwa wakati wote kama ilivyokusudiwa.

“Naunda timu ya watu watatu, mmoja kutoka hapa na wawili Katibu Mkuu wa Ujenzi atawateua kutoka wizarani ili iniambie ni nini hasa kinaendelea hapa Pangani, haiwezi ikawa kila siku wananchi wanapata usumbufu”, amesisitiza Ulega.

Ulega amefanya maamuzi hayo kutokana na Kivuko hicho cha MV TANGA kushindwa kufanya kazi kwa siku nne huku watendaji na wasimamizi wakishindwa kufanya maamuzi ya haraka ya upatikanaji wa vipuri vya kufungwa katika kivuko hicho na kusisitiza kuwa endapo itabainika kuna hujuma zinafanyika katika kivuko hicho atachukua hatua za kinidhamu.

Naye Mbunge wa Jimbo la Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya usafiri wa Kivuko cha MV TANGA ambacho ni muhimu na msaada kwa wananchi wa Pangani.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa.

No comments:

Post a Comment