
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na wataalaam wenye utaalam wa juu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili iweze kutoa huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni kushika nafasi mbalimbali katika viwanja vya Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.
Rais Dkt. Samia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo kuendelea kusimamia utoaji wa huduma katika hospitali hiyo kubwa na kongwe, kiongozi katika matibabu ya ubingwa bobezi na utalii tiba katika Kanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Muhimbili inahitaji professionalism na administative skills, nenda kaendeleze pale alipoishia Prof. Janabi, nimepitia wasifu wa watu wengi lakini nikaona wewe Dkt. Delilah Kimambo ndio unafaa kuiongoza hospitali hiyo, nakutakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yako” ameongeza Rais Dkt. Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali imepata fedha kwa ajili ya maboresho ya hospitali hiyo husani katika eneo la ujenzi wa miundombinu ya majengo ikiwa ni muendelezo wa mikakati ya kuboresha sekta ya afya hapa nchini.
Dkt. Delilah Kimambo aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Juni 16, 2025.

No comments:
Post a Comment