NJAMASII CHIWANGA ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA MPWAPWA KUPITIA CCM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 28, 2025

NJAMASII CHIWANGA ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA MPWAPWA KUPITIA CCM



Na Barnabas Kisengi, Mpwapwa


Ikiwa ni siku ya kwanza tangu kufunguliwa kwa dirisha la uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi ya ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya watia nia wameanza kujitokeza kuchukua fomu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma.

Katika ofisi za CCM Wilaya ya Mpwapwa, mmoja wa watia nia, Ndugu Njamasii Chiwanga, amejitokeza na kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge kwa Jimbo la Mpwapwa kupitia chama hicho tawala.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi fomu hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Mpwapwa, Ndugu Denes Luhende, amesema fomu hiyo ina maelekezo yote muhimu, hivyo ni wajibu wa mtia nia kuijaza kwa umakini na kuiwasilisha kwa mujibu wa taratibu za chama.

“Fomu hii imeeleza kila kitu kinachotakiwa, hivyo tunaamini utaitumia kwa makini na kuiwasilisha kama inavyoelekezwa kwenye maelekezo ya chama,” amesema Katibu huyo.

Kwa upande wake, Ndugu Njamasii Chiwanga amesema amejipima kwa kina na kuona anazo sababu za msingi zinazompa uhalali wa kuomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Mpwapwa kupitia nafasi ya ubunge.

"Nilijitafakari kwa umakini sana na kuona nina uwezo wa kushika hii nafasi ya ubunge kwa kupitia chama changu cha Mapinduzi. Hivyo leo, Juni 28, 2025, nimechukua fomu hii. Kwa kuwa CCM kina utaratibu wa vikao vyake, baada ya kurejesha fomu, nitasubiri kwa heshima taratibu za chama," amesema Chiwanga.

Zoezi la uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM limezinduliwa rasmi leo, Juni 28, 2025, na linatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025.

No comments:

Post a Comment