
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dar es Salaam wamefanya ukaguzi wa ujenzi na matengenezo ya barabara katika mkoa huo unaolenga kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango na kwa wakati.
Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga amesema kuwa, wametembelea wilaya ya Temeke ambapo walikagua barabara mbalimbali ikiwemo barabara ya kwa Diwani na zile zinazotekelezwa chini ya mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP).

“Tumeona maendeleo mazuri kwenye utekelezaji, Mkandarasi yupo kazini na tunatarajia kujenga zaidi ya Km 7.2 katika eneo la makazi na biashara, ambapo magari makubwa na malori hupita mara kwa mara. Barabara zinajengwa kwa kiwango cha zege ili kukidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi zinazofanyika", amesema Mkinga.
Pia alitembelea barabara ya Yombo yenye urefu wa Km 1.6, ambapo ujenzi unaendelea kwa kiwango cha zege katika maeneo ya wazi pamoja na kipande cha mita 600 kinachojengwa kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke.
“Ninamshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za matengenezo. Hii imerahisisha utekelezaji wa barabara ya Yombo na ile ya Dkt. Omar. Kipande cha mita 600 kinachojengwa chote kwa zege”, ameongeza.
Meneja Mkinga pia alitembelea barabara ya Tuangoma–Masaki yenye urefu wa Km 3.9, eneo ambalo awali lilikuwa na changamoto kubwa ya mvua na udongo laini uliokuwa ukisababisha kukatika kwa mawasiliano.
“Hili ni eneo la mchanga, mvua ikinyesha tu hakuna mawasiliano kabisa. Mkandarasi anayetekeleza mradi huu anafanya kazi chini ya mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 27. Mradi unahusisha pia ujenzi wa vivuko vya Chaulembo ambavyo vimepangwa kwa mujibu wa maelekezo ya viongozi wa mkoa”, amesema.
Akiwa eneo la Chamaruba, ameeleza namna mvua kubwa za Aprili na Mei zilivyoharibu miundombinu na kufunga kabisa mawasiliano kati ya pande mbili za mtaa huo. Hata hivyo, kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali ya Mtaa na Serikali Kuu, fedha za dharura zilitolewa ili kujenga makalavati matano na kurudisha mawasiliano.
Kwa upande wao, wananchi wa maeneo hayo walitoa shukrani zao kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi hiyo ambayo imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi.
“Awali ilikuwa tunapata shida kuwavusha watoto kwenda shule, hadi mzazi umpeleke mtoto na umrudishe. Wakati mwingine wagonjwa walihitaji kubebwa hadi upande wa pili. Lakini sasa hivi, tuna daraja, tuna barabara, tuna amani, tunaishukuru serikali", amesema mmoja wa wakazi wa eneo la Chamaruba.








No comments:
Post a Comment