FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI-MAJALIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 18, 2025

FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa Sera kuwekeza katika tafiti zenye tija kwa wananchi.



Amesema kufanya hivyo, kutawezesha kuwa na matokeo ambayo yatatumika kutengeneza sera na mipango ya utekelezaji yenye kuleta mabadiliko halisi katika jamii.

Ametoa wito huo leo Jumatano (Juni 18, 2025) kwenye Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika chuoni hapo kampasi ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam.
 



“Tunataka kuona matokeo ya tafiti hizi yanatumika, msiweke tafiti hizi kwenye makabati tu, matokeo haya yanapaswa kuleta tija katika sekta ya afya, Ni matarajio yangu kuwa kongamano hili litatumika kutoa mapendekezo yatakayoimarisha mifumo, sera, na ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na mapinduzi haya”




Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba, na teknolojia mpya ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na magonjwa kwa wakati.




Amesema kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu, rasilimali watu, tiba za kibingwa, na mifumo ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

 “Tutaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, salama na rafiki bila kujali mahali alipo”.




Pia, Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoomgozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba ndani ya nchi.


 “Tayari tumeanza kushuhudia hatua chanya katika maeneo haya, tukijivunia mchango wa wataalamu wetu wa ndani”.



“Serikali yetu imeendelea kuimarisha mazingira ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya. Leo hii, hospitali zetu zinatumia mifumo ya kidijitali kubaini magonjwa, kutoa tiba sahihi, na kufuatilia maendeleo ya wagonjwa.”




Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Serikali imeweka vipaumbele kwenye elimu, sayasi na teknolojia. 


“Tunajivunia mageuzi makubwa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, uongozi wake umeleta mageuzi mapya katika kuimarisha taasisi za elimu nchini”.




Amesema kuwa maboresho yaliyopo chuoni hapo ni ushahidi mkubwa wa namna serikali inavyoweka mipango ya kuboresha mazingira ya Ujifunzaji na Kufundishia.




Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Appolinary Kamuhabwa Ameipongeza Serikali kwa jitihada za dhati ambazo zimewezesha kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoleta mageuzi makubwa katika mazingira ya elimu ya juu na afya nchini.

Prof. Appolinary amesema ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki (yaani "East African Centre of Excellence for Cardiovascular Sciences") unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni moja ya miradi itakayotekelezwa.




“Mradi huu unaingia katika awamu ya pili, baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hiki muhimu hapa Mloganzila, Awamu ya kwanza iligharimu shilingi bilioni 21.62 na Awamu ya pili ya mradi huu ambayo imeanza rasmi mwezi Mei 2025, inalenga kujenga Hospitali ya Kisasa ya Kufundishia wataalamu bingwa na bobezi wa magonjwa ya Moyo na Mishipa ya damu”. Alisema Prof. Appolinary



Amesema kuwa Hospitali hiyo itakaongeza
uwezo wa kutoa huduma za kibingwa, kufundisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi, na kufanya tafiti zinazolenga kukabiliana na changamoto za magonjwa ya moyo na mishipa.

“Awamu hii itagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 221.57.”

No comments:

Post a Comment