MICHEZO KICHOCHEO CHA UPENDO NA USHIRIKIANO MAHALA PA KAZI - MAVUNDE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 28, 2025

MICHEZO KICHOCHEO CHA UPENDO NA USHIRIKIANO MAHALA PA KAZI - MAVUNDE



Na Okuly Julius – Dodoma


Watumishi wa Wizara ya Madini wametakiwa kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mchango mkubwa wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, hasa wakati huu ambapo mwaka mpya wa fedha umeanza kwa malengo mapya na mikakati madhubuti.

Wito huo umetolewa leo Juni 28, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati wa Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Taasisi zake, lililofanyika Jijini Dodoma kwa lengo la kuimarisha afya za watumishi, kuhamasisha mshikamano na kukuza ari ya kazi.


“Nyie ndio mnaifanya sekta yetu kuonekana. Tuendelee kujijenga kwa upendo kama timu moja imara. Mwaka huu mpya wa fedha tunaelekea kuuanza tukiwa na malengo mazuri, naomba tuendelee kufanya kazi kwa moyo mmoja,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Akizungumzia kauli mbiu ya wizara hiyo ya "Madini ni Maisha na Utajiri", Waziri Mavunde amesema inadhihirisha mafanikio yanayopatikana kupitia juhudi kubwa za watumishi wa sekta hiyo. Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha mazingira bora ya kiutendaji katika sekta ya madini.

"Tunamshukuru sana Rais kwa kutuwezesha kutimiza malengo ya sekta, ambapo kupitia uongozi wake, sekta ya madini imepiga hatua kubwa. Pia nampongeza Katibu Mkuu kwa kuwaongoza watumishi kwa weledi, nidhamu na mshikamano,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Ismail Samamba, amesema bonanza hilo ni utekelezaji wa agizo la Waziri la kuhimiza mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuimarisha afya na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza, huku likilenga pia kuongeza tija kazini.

“Mazoezi ni msingi wa afya bora. Kupitia bonanza hili tunajenga afya, ushirikiano na pia tunatekeleza maelekezo ya Waziri pamoja na kusimamia dira ya Serikali inayohimiza utumishi wenye afya na tija,” amesema Samamba.

Ameongeza kuwa bonanza hilo linahitimisha mwaka wa fedha 2024/2025, na kuwa utaratibu huo utaendelezwa ili kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi wa Wizara na Taasisi zake.

Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahaman Mwanga, amempongeza Waziri Mavunde kwa uongozi wake mahiri ambao amesema umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya madini na kuwapa watumishi motisha ya kufanya kazi kwa bidii.

Bonanza hilo lilijumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, kuvuta kamba na mbio, ambapo watumishi walishiriki kwa furaha na mshikamano mkubwa, wakitumia fursa hiyo kusherehekea mafanikio ya pamoja na kujipanga kwa mwaka mpya wa kazi.














No comments:

Post a Comment