Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kuimarisha utendaji kazi na hivyo kuifanya Sekta ya Nishati kuwa na matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo kufuatia tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati ambayo imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa Wizara/Taasisi umeimarika kwa zaidi ya asilimia 95.
Katika kikao cha Nne cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilichofanyika jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema kuwa, tathmini hiyo inasaidia kujiimarisha hasa ikizingatiwa kuwa Sekta ya Nishati ina muhimu mkubwa kiuchumi na kijamii.
“Sekta hii ni muhimu sana nchini kwa kuwa ni Sekta ya huduma na sekta ya uchumi hivyo ikilegalega italeta malalamiko, ningependa kuona sekta hii inaendelea kuwa na matokeo mazuri kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko
Katika kikao hicho, Dkt. Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea na kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya umeme.
Aidha, ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kasi iliyofanya ya kupeleka umeme vijijini na kuwezesha vijiji vyote kupata umeme pia kwa kuendelea na kasi ya kupeleka umeme vitongojini.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara hususan, REA, TPDC na TANESCO kuunganisha nguvu katika kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ili ikue na kufanikiwa na hivyo kutimiza lengo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka matumizi ya Nishati isiyo safi kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Dkt. Biteko amekipongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati kwa kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi na kukumbusha Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuwa, zoezi hilo la tathmini linapaswa kuwa ni endelevu kutokana na umuhimu wake katika kuboresha utendaji kazi.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith.Kapinga kwa upande wake, amezipongeza Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Nishati kwa utendaji kazi wenye kuleta matokeo kama ambavyo tathmini ya utendaji kazi iliyotolewa ilivyoonesha kuwa ufanisi wa kazi umeendelea kuimarika.
Aidha amezitaka Taasisi chini ya Wizara ya Nishati kuibeba Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ili kufikia lengo la Serikali la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kuwa kikao hicho cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara na Taasisi zake ni cha nne kutoka vikao vivyo vimeanza kufanyika.
Alieleza kuwa, kutoka zoezi la kupima utendaji kazi wa Wizara na Taasisi lianze kufanyika limeleta ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na mipango ya Wizara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Sakina Mwinyimkuu ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutekeleza miongozo iliyowekwa na Ofisi hiyo ya ufuatiliaji na tathmini ambapo ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imetekeleza miongozo iliyowekwa kwa asilimia 100.
Pia amempongeza Dkt. Doto Biteko kwa dhamira yake ya dhati katika kusimamia utendaji kazi wa Serikali hasa Sekta ya Nishati ambayo anaisimamia akiwa ni Waziri wa Nishati.
Vilevile, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutoa motisha kwa Taasisi na Idara/Vitengo zilizofanya vizuri zaidi katika tathmini ya utendaji kazi hali ambayo inaongeza ari ya kazi.
Taasisi zilizofanya vizuri Katika tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika katika robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ni Wakala wa Nishati Vijijini (REA) aliyeshika nafasi ya kwanza, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) aliyeshika nafasi ya pili na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) aliyeshika nafasi ya tatu.
Aidha, Idara/Vitengo vya Wizara ya Nishati vilivyofanya vizuri Katika tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika katika robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ni Kitengo cha Ugavi na Manunuzi (nafasi ya kwanza), Kitengo cha Sheria (nafasi ya pili), na Kitengo cha TEHAMA (nafasi ya tatu).
Mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika tathmni ya utendaji kazi ni Manyara (nafasi ya kwanza), Arusha (nafasi ya pili) na Simiyu (nafasi ya tatu).
Hata hivyo ilielezwa kuwa kwa ujumla ufanisi wa utendaji kazi wa Idara na Vitengo vya Wizara pamoja na Taasisi zake umeendelea kuimarika kwa zaidi ya asilimia 95.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt, James Mataragio, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake pamoja na Mameneja wa Mikoa wa TANESCO.
No comments:
Post a Comment