Na John Mapepele
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa rai kwa walimu nchini kuwa wazalendo na kuzingatia weledi wao ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Mhe. Mchengerwa alitoa rai hiyo wakati wa mkutano wa walimu na wadau wa elimu wa Wilaya ya Rufiji, uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bibi Titi Mohamed, ambapo pia alitunukiwa tuzo ya heshima kutambua mchango wake katika sekta ya elimu wilayani humo.
"Katika hali ya kawaida, Serikali imeboresha mazingira na miundombinu ya sekta ya elimu. Kilichobaki ni kwa sisi walimu kutanguliza uzalendo ili kuinua kiwango cha elimu katika ngazi zote," alisisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha, aliwataka walimu kutambua wajibu wao kikamilifu na kusisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya walimu na maafisa elimu watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katika taarifa ya Wilaya ya Rufiji iliyowasilishwa kwa Mhe. Waziri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Simon Berege, imeelezwa kuwa kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kutoka 3,135 mwaka 2020 hadi 3,715 mwaka 2024.
Vilevile, idadi ya shule za awali na msingi imeongezeka kutoka 48 mwaka 2021 hadi 63 mwaka 2025, ongezeko la shule 15 sawa na asilimia 31.3.
Vyumba vya madarasa pia vimeongezeka kutoka 377 mwaka 2021 hadi 566 mwaka 2025, ongezeko la vyumba 189 sawa na asilimia 50.1.
Katika mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa, Halmashauri ya Mji wa Rufiji iliibuka mshindi wa kwanza katika michezo ya mpira wa miguu, pete na riadha, huku ikishika nafasi ya pili kwenye mpira wa mikono, na hivyo kushika nafasi ya pili kwa ujumla katika mashindano hayo.
Katika mkutano huo, Mhe. Waziri Mchengerwa alikabidhi makombe kwa shule zilizoshinda na baadaye alipokea msaada wa madawati 50 yaliyotolewa na Benki ya CRDB.
No comments:
Post a Comment