WIZARA YA FEDHA YAOMBA KUIDHINISHIWA TRILIONI 20.19 KWA MATUMIZI YA 2025/26 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 4, 2025

WIZARA YA FEDHA YAOMBA KUIDHINISHIWA TRILIONI 20.19 KWA MATUMIZI YA 2025/26


Wizara ya Fedha imewasilisha ombi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuidhinishiwa matumizi ya jumla ya Shilingi trilioni 20.19 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Kati ya fedha hizo ,Shilingi trilioni 19.43 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi trilioni 1.10 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi trilioni 18.33 ni kwa matumizi mengineyo.

Waziri wa fedha Dkt.Mwigulu Nchemba akizungumza leo June 4,2025 Bungeni Dodoma amesema Shilingi bilioni 757.79 zitaelekezwa kwenye matumizi ya maendeleo.

Amesema Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi nayo imeomba kuidhinishiwa Shilingi bilioni 122.52, ambapo Shilingi bilioni 110.42 ni kwa matumizi ya kawaida,Shilingi bilioni 12.10 ni kwa matumizi ya maendeleo.

Kuhusu Mapato Yanayotarajiwa Kukusanywa,Waziri huyo wa Fedha amesema ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo, Wizara ya Fedha imekadiria kukusanya jumla ya Shilingi trilioni 50.17 kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje.

Aidha Mchanganuo wa mapato hayo ni Shilingi trilioni 34.10 zinatarajiwa kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama mapato ya kodi na yasiyo ya kodi huku Shilingi trilioni 1.07 ni misaada ya wahisani.

"Shilingi trilioni 14.95 ni mikopo ya masharti nafuu na ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi,Shilingi bilioni 53.54 ni maduhuli ya serikali,aidha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inatarajiwa kukusanya Shilingi milioni 843 kutoka ukodishaji wa kumbi na upangishaji wa majengo ya serikali katika mikoa mbalimbali, "amesema.

Akichangia mara baada ya Waziri kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Viti Maalum Subira Mgalu amepongeza hatua ya serikali kuweka malengo makubwa ya mapato, akisema ni hatua ya kuimarisha uchumi wa ndani na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.

Kuhusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya zaidi ya Shilingi trilioni 34.10 kwa mwaka wa fedha 2025/2026,Mbunge huyo amesema bado kunahitajika hatua madhubuti za kuongeza ufanisi na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.

"TRA imefanya kazi kubwa, lakini bado tuna changamoto katika maeneo ya mipakani, biashara zisizosajiliwa na matumizi hafifu ya mifumo ya kidijitali. Tunaiomba Serikali kuhakikisha mifumo kama TANCIS na IDRAS inaboreshwa zaidi na inatumika ipasavyo," amesema mbunge huyo.

Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia si tu yatapunguza mianya ya ukwepaji kodi, bali pia yataongeza uwazi, kupunguza mwingiliano kati ya wakusanyaji na walipa kodi na kuongeza imani ya walipa kodi kwa serikali.

Aidha, ameshauri TRA kuwekeza zaidi katika elimu ya kodi kwa wananchi, hasa wafanyabiashara wadogo, akisema: “Kuna watu wanakwepa kodi si kwa nia mbaya, bali kwa kutofahamu wajibu wao.”ameeleza na kusisitiza ;

“Wajasiriamali bado wanakabiliwa na changamoto za tozo na urasimu, hivyo TRA inapaswa kujikita zaidi kwenye elimu ya kodi na usimamizi jumuishi badala ya kushinikiza tu ukusanyaji,” amesema.

Mjadala wa bajeti unaendelea huku wabunge wakisisitiza umuhimu wa kuongeza mapato ya ndani kwa njia endelevu, rafiki kwa walipa kodi na yenye tija kwa maendeleo ya wananchi.


No comments:

Post a Comment