
Na Mwandishi Wetu, Mlele, Katavi
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambayo itaondoa kero ya miundombinu isiyopitika katika kijiji cha Kalovya kata ya Inyonga wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Meneja wa TARURA wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya, amesema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa km 1.5 imegharimu zaidi ya shilingi milioni 838 ikihusisha ujenzi wa mitaro ya maji pamoja na ujenzi wa kalavati sita.
Mhandisi Mabaya amesema fedha za ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya tozo za mafuta.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ndugu Ismail Ali Ussi amesema serikali itaendelea kujenga barabara na madaraja ili kila mwananchi aweze kufungua fursa za kiuchumi.
Bi. Hawa Shijja, mkazi wa kijiji cha Kalovya ameishukuru serikali kwa barabara hiyo ya kiwango cha lami na kusema kwamba itasaidia kwenye usafirishaji wa mazao kwenda sokoni kwani sehemu kubwa ya wananchi wa maeneo hayo ni wakulima.



No comments:
Post a Comment