MAJALIWA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE JIMBO LA MCHINGA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 7, 2025

MAJALIWA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE JIMBO LA MCHINGA.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 07, 2025 amezindua kampeni za Ubunge jimbo la Mchinga zilizofanyika katika kijiji cha Rutamba mkoani Lindi

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 imejielekeza katika kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini ikiwemo katika jimbo la Mchinga.

“Katika kipindi kilichoisha Rais Dkt. Samia ameleta hapa miradi mikubwa, ya kati na midogo, anafanya hivi kwa kutambua wananchi wanapaswa kuhudumia, hata ilani hii imeonesha maeneo mengine yatakayotekelezwa katika mkoa huu wa Lindi”

Amesema kuwa Wana-Lindi wanapaswa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa barabara ya Dar-Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi, ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika.

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Lindi, ilani hii imeendelea kusheheni miradi inayokwenda kutekelezwa katika maeneo yetu, hii ni sababu pekee ya sisi kumchagua Rais Dkt. Samia.

“Ilani ya uchaguzi ya 2025/2030 imeonesha kuwa kutaanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo-Ng’apa, Mandawa hadi Chikundi, barabara hii itakuwa ni mkombozi kwa wakati wa wakazi wa maeneo haya na itafungua uchumi kwa Wana-Lindi.”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo hilo limefanikiwa kuwa na magari ya wagonjwa Manne pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha huduma za afya katika jimbo hilo.

“Mheshimiwa Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia wananchi, kwa namna jimbo hili lilivyokaa linahitaj mtu mahiri na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake, hakika Mheshimiwa Salma ameonesha ameweza, mchagueni tena”

Kwa Upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo Salma Kikwete amesema kuwa katika katika kipindi chake amefanikiwa kushirikiana na WanaMchinga kutafuta majibu ya changamoto yaliyo katika jimbo hilo

“Tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto zetu, hali ilivyo leo sio sawa na tulikotoka, tumepata mafaniko katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, nishati, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, nikipata ridhaa tena tutafanya makubwa zaidi”

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano amefanikiwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ng’apa ambao utawezesha kuvifikia vijiji vingi katika jimbo la Mchinga. “kama hiyo haitoshi tumefanikiwa kujenga zahanati, tutaongeza juhudi za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya”

Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwa anatosha katika nafasi ya Urais, kwani katika kipindi kifupi amefanya mambo mengi
tumpe nafasi aendelee

“Alipata Urais katika wakati ambao hakutarajia, lakini amefanya kazi nzuri, tutanufaika mara dufu, tukimpa nafasi, nimeangalia orodha ya mambo yaliyo kwenye ilani kwa hakika amejipanga”

Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge mkoa wa Lindi, Mgombea ubunge jimbo la Mtama Nape Nnauye amesema kuwa wanakusini watamchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika mkoa huo ikiwemo utoaji wa Ruzuku ya pembejeo kwenye mazao.









No comments:

Post a Comment