
Na Mwandishi Wetu, Geita
Katika ulimwengu wa uchimbaji mdogo, changamoto kubwa imekuwa namna ya kupata dhahabu kwa ufanisi na gharama nafuu, bila kupoteza rasilimali nyingi wala uharibifu wa mazingira na ukitumia vifaa vya kawaida na nishati kidogo kulinganisha na CIP zilizozoeleka.
Miaka kadhaa iliyopita, wachimbaji wadogo walihangaika, dhahabu nyingi ilibaki kwenye udongo, gharama za uchenjuaji zikiwa kubwa, na uharibifu wa mazingira ulionekana kutokana na njia za kijadi za kuchejulia dhahabu.
Lakini sasa, simulizi ya ubunifu wa mtambo wa uchenjuaji madini ya dhahabu (CIP) inayotengenezwa kwa gharama nafuu ni teknolojia inayochenjua dhahabu kwa zaidi ya asilimia 98%.
Mtambo huo ambao umetengezwa tofauti kidogo na ile iliyozoeleka umekuwa mkombozi wa wachimbaji wadogo.
Unapowekwa udongo wenye dhahabu ndani yake, dhahabu inatoka kwa usahihi, ufanisi, na kinachobaki ni udongo usio na madhara makubwa kwa mazingira.
John Ngeda, ni mmoja wa wabunifu wa mtambo huo, anasema kuwa, safari yake ya maarifa ilimpeleka nchini Zimbabwe, ambako alijifunza mbinu za uchenjuaji, kisha akaamua kurudi nyumbani na kuboresha teknolojia hiyo kwa manufaa ya wachimbaji wa Tanzania.
Matokeo yake yamekuwa makubwa kwani zaidi ya mitambo 25 imejengwa katika Kanda ya Ziwa pekee, na sasa ipo hadi Mbeya na Mpanda.
Wachimbaji wadogo wanaona utofauti si tu kwamba wanapata dhahabu zaidi, bali pia wanaokoa gharama kubwa walizokuwa wakitumia kwa njia zisizo na tija. Mazingira pia yanapumua, kwa sababu teknolojia hii ni rafiki wa mazingira, ikipunguza madhara yaliyokuwa yakisababishwa na kemikali hatarishi.
Katika Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini Geita tarehe 23 Septemba 2025, mtambo wa CIP umegeuka kivutio kikuu.
Wananchi wanapata kushuhudia jinsi teknolojia hiyo ilivyobadilisha maisha ya wachimbaji wadogo kutoka hali ya kuchimba kwa mazoea na hatimaye kuchimba kwa tija zaidi.
Hii siyo tu simulizi ya dhahabu, bali ni simulizi ya ubunifu wa Mtanzania, na ushindi wa teknolojia rafiki kwa binadamu na mazingira.
Dhahabu sio ndoto au madini yanayoambatana na ushirikina bali ni urithi unaleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi pia huku ikibadili maisha ya maelfu.
Dhahabu haipo tu ardhini; ipo pia kwenye mawazo ya wabunifu wanaothubutu.








No comments:
Post a Comment