
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Septemba 06, 2025 akiwa Mafinga Mkoani Iringa amesema Mkoa huo ni Miongoni mwa Mikoa itakayonufaika na ahadi ya CCM ya kujenga Kongani za Viwanda kwa Vijana ili kuongeza thamani ya mazai ya Kilimo na ufugaji nchini.
"Iringa hii ina kilimo lakini pia ina uvunaji wa misitu na moja katika kongani tuliyoifikiria ni kongani ya mazao ya misitu, kwahiyo tutafikiria Wilaya gani kongani ya Viwanda ikae ili Vijana waongeze thamani mazao ya misitu na waweze kutumia soko la ndani lakini soko la Kimataifa kuuza bidhaa zao." Amesema Dkt. Samia.
Akizungumza na Maelfu ya wanachama wa CCM na wananchi wa Mji wa Mafinga, Dkt. Samia pia amesisitiza kuwa Serikali yake ikiwa atapata ridhaa ya kuongoza tena watanzania, ataendeleza sera yake ya ruzuku kwenye sekta ya Kilimo na ufugaji kwa kuendelea kutoa ruzuku kwenye bei za pembejeo, Mbolea na mbegu pamoja na ruzuku ya chanjo kwenye mifugo katika jitihada za kuongeza uzalishaji zaidi wa mazao ya chakula na mifugo.
Aidha kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya Biashara, Dkt. Samia amesisitiz kuwa serikali yake itaendelea kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula NFRA pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao hayo ili kuepukana na uharibifu na upotevu wa mazao msimu wa mavuno kwa wakulima.


No comments:
Post a Comment