
Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kupuuza upotoshaji unaoenezwa kwenye Mitandao ya kijamii kuhusu uchapishaji wa fedha mpya kutokana na serikali kuishiwa fedha, akisema kwasasa Serikali ina akiba ya zaidi ya Trilioni 16 na hakuna nchi yoyote duniani yenye mtambo wake binafsi wa uchapishaji wa fedha.
Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 19, 2025 wakati wa Kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM huko Wilayani Mpanda Mkoani Katavi kwenye vya Azimio, akiwaomba Watanzania kujiepusha na wote wanaoelekeza mambo mabaya dhidi ya Tanzania.
"Wengine wanasema kwamba serikali imeishiwa inaprint hela. Moja, tuna akiba ya zaidi ya trilioni 16, mbili, hakuna nchi hata moja inayomiliki mtambo wake wa kuchapisha pesa ili itumie yenyewe. Fedha utaratibu wake mpaka ichapishwe inakuchukua miaka miwili, utawezaje kuchapisha fedha baada ya kuingia kwenye uchaguzi? Wanadhani fedha unatoa photocopy, karatasi ya fedha sio ya photocopy wala hamna nchi yenye mashine ya photocopy ya kuchapisha fedha." Amesisitiza Waziri Mwigulu.
Katika hatua nyingine akirejea maandiko ya Biblia, Mwigulu amewataka watanzania kuwakataa wale wote wanaochochea wengine kufanya fujo, akisema hakuna nchi mbadala wa Tanzania, akiwataka wote kudumisha amani ya Tanzania na kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi CCM, katika uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025.


No comments:
Post a Comment