WENJE AWASHANGAA WANAODAI DKT. SAMIA ANAKANDAMIZA DEMOKRASIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 18, 2025

WENJE AWASHANGAA WANAODAI DKT. SAMIA ANAKANDAMIZA DEMOKRASIA


Mwanachama Mpya wa Chama Cha Mapinduzi Ezekiah Wenje amesema katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya kesi 417 ikiwemo sita za Mwenyekiti wa sasa wa Chadema Tundu Lissu zilifutwa na kuondolewa mahakamani kama sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya 4R iliyokuwa ikisisitiza pamoja na mambo mengine kuhusu maridhiano na kujenga upya.

Wenje amebainisha hayo leo Oktoba 18, 2025 wakati akizungumza na kumnadi Mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan huko Namanyere, kwenye Viwanja vya sabasaba, Nkasi Mkoani Rukwa, akionesha kushangazwa na wanaomshambulia Dkt. Samia na wanaodai kuwa serikali yake imeminya demokrasia kwa Vyama vya siasa.

Wenje amesema baada ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania yeye, Godbless Lema na aliyekuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema Bw. Tundu Lissu walikimbia nchi kutokana na yaliyokuwa yakiendelea na ni Dkt. Samia aliyewafungulia tena milango ya kurejea nchini bila ya masharti yoyote na akiwaruhusu kufanya Mikutano ya kampeni na Maandamano sambamba na kutoa uhuru wa kutoa maoni na kukosoa kwa Wanasiasa na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi.

"Mhe. Rais, Mwenyekiti wa wakunja ngumi mwenyewe binafsi alikuwa na kesi sita na zote zilifutwa, kwenye Chama zilikuwepo kesi 419 za wanachama na kwa haraka sana kesi hizi ziliondoka, hivi Kama haya yalifanyika? Demokrasia na mtu mwema ni yupi? Mikutano pia iliruhusiwa nchi nzima, tukafanya nchi nzima na bado tukamtukana, hivi demokrasia ni nini?" Amehoji Ndugu Wenje.

Wenje ameeleza pia kuhusu ruzuku kwa Chama chake cha zamani Chadema, akisema mara baada ya Chadema kususia ruzuku hiyo ya serikali, Chama kilipitia wakati mgumu kiuchumi na kushindwa kujiendesha na Dkt. Samia pia ndiye aliyeruhusu Chama hicho kuendelea tena kupokea ruzuku, ruzuku iliyosaidia katika ununuzi wa Majengo yanayotumiwa kama Makao makuu ya Chama hicho yaliyopo Mikocheni Jijini Dar Es Salaam.

Katika hatua nyingine Wenje amewataka wanaokosoa na kudai kuwa hakuna maendeleo yaliyofanyika chini ya Serikali ya awamu ya sita kutenga muda wa kufanya utafiti kuhusu hatua kubwa zilizofanyika, akidai kuwa kwa kanuni za kawaida kabisa namba huwa hazidanganyi na yapo mambo mengi yenye kuonekana kwa macho ya kawaida ikiwemo reli ya kisasa ya SGR ambayo inatumika na watu wote ikiwemo watu hao wanaoikosoa serikali ya awamu ya sita.




No comments:

Post a Comment