EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Sahara Ventures imezindua rasmi programu ya kitaifa ya kuharakisha ukuaji wa biashara changa na kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini.
Programu hiyo inalenga kuwaunganisha wabunifu, watafiti, wawekezaji, sekta binafsi pamoja na taasisi za serikali ili kusaidia kukuza biashara bunifu zinazoanzishwa na vijana.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika Machi 12, 2026 katika makao makuu ya COSTECH jijini Dar es Salaam na kuwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za serikali, vyuo vikuu, vituo vya ubunifu, sekta binafsi, wawekezaji, washirika wa maendeleo pamoja na wajasiriamali.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema programu hiyo itatekelezwa kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na inalenga kufikia makampuni madogo ya vijana zaidi ya 1,000 ndani ya kipindi cha miaka minne.
Amesema kila mwaka programu hiyo itasaidia makampuni 250 yanayomilikiwa na vijana, huku ikianza kwa kuangazia sekta sita ambazo ni madini, nishati, utalii, kilimo, viwanda na teknolojia.
“Tutawezesha kampuni 250 zinazomilikiwa na vijana kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne. Tutafanya kazi kwa karibu na wizara za sekta husika ili kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za serikali katika kufungua fursa ndani ya sekta hizo. Vijana wenye mawazo bunifu na makampuni yao watapata nafasi ya kuchaguliwa na kunufaika na programu hii,” amesema Mtambalike.
Amesema malengo ya programu hiyo ni kuharakisha ukuaji wa biashara changa zenye ubunifu, kusaidia kubadilisha matokeo ya tafiti kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuwa bidhaa na huduma za kibiashara, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, vyuo vikuu, sekta binafsi na wawekezaji.
Aidha, amesema programu hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa mitaji na fursa za uwekezaji kwa biashara changa na kuongeza ushindani wa kimataifa wa biashara za ubunifu kutoka Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Amosi Nungu amesema programu hiyo ni muhimu kwa kuwa biashara nyingi changa hukosa msaada maalumu wa kiufundi na kifedha unaoweza kuzisaidia kukua.
Amesema mara nyingi matokeo ya tafiti kutoka vyuo vikuu hubaki maabara badala ya kufikishwa sokoni, huku wajasiriamali wachanga wakikumbana na changamoto ya kupata mitaji na masoko.
“Mpango huu hauhusu tu kusaidia biashara changa, bali ni juhudi za kuimarisha mfumo wa kitaifa wa ubunifu unaoratibiwa kikamilifu. Serikali inaweka sera na miongozo ya mazingira wezeshi, vyuo vikuu vinatoa tafiti na utaalamu wa kitaaluma, sekta binafsi inafungua masoko na ushirikiano wa kibiashara, wawekezaji wanatoa mitaji huku washirika wa maendeleo wakisaidia kuimarisha mfumo mzima wa ubunifu,” amesema Nungu.
Naye Mkurugenzi wa Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), Patience Karua amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Sahara Ventures imejipanga kuhakikisha programu hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa biashara bunifu nchini.
Amesema programu hiyo itasaidia vijana wenye biashara zao kupata nafasi nzuri katika masoko pamoja na kuvutia wawekezaji.

No comments:
Post a Comment