TAMISEMI YASHAURIWA KUFUATILIA UBORA WA VYAKULA VINAVYOUZWA MAENEO YA SHULE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 12, 2026

TAMISEMI YASHAURIWA KUFUATILIA UBORA WA VYAKULA VINAVYOUZWA MAENEO YA SHULE

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.

Sehemu ya wanafunzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.

Sehemu ya wanafunzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.

Wanafunzi wakisoma risala pamoja na kucheza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika leo Machi 12, 2026, jijini Dodoma.


Na.Okuly Julius, OKULY BLOG -DODOMA

Watendaji katika Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wameshauri kuendelea kufuatilia vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya shule ili kuhakikisha vinakuwa salama kwa matumizi ya wanafunzi na vinaendana na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu afya ya umma.


Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni yaliyofanyika Machi 12, 2026 jijini Dodoma.

Mhe. Ameir amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kuwahimiza wadau wa elimu kuunga mkono mpango wa utoaji wa chakula mashuleni, hatua inayolenga kuboresha mahudhurio, ufaulu wa wanafunzi, afya pamoja na maendeleo yao wakiwa shuleni.

Amesema mpango wa chakula shuleni una mchango mkubwa katika kuboresha afya na uwezo wa wanafunzi kujifunza, kwa kuwa watoto hutumia muda mwingi wakiwa shuleni kuliko nyumbani.

Aidha, amesisitiza kuwa upatikanaji wa chakula bora, maji safi na mazingira salama ya usafi ni mambo muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ameir amewataka wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha miundombinu muhimu shuleni ikiwemo ujenzi wa stoo za chakula, mabwalo ya kulia chakula, majiko ya kupikia, matumizi ya nishati safi pamoja na vituo vya kunawia mikono.

"Nawahimiza wazazi kushirikiana na shule kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya chakula wakiwa shuleni kama ilivyoelekezwa katika Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2016," amesema.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango wa chakula na lishe shuleni unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, maji, maendeleo ya jamii pamoja na wadau wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Pia amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Chakula Bora, Maji Safi Shuleni: Ni Wajibu wa Pamoja,” inayolenga kuhamasisha ushirikiano wa Serikali, wadau wa maendeleo na jamii katika kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma muhimu shuleni ikiwemo chakula, maji safi na huduma za afya.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo, Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Bi. Christin Mendezi, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha na kupanua mpango wa utoaji wa chakula mashuleni.

Amesema mpango huo una mchango mkubwa katika kuboresha afya, mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi.

Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, mpango wa chakula shuleni unaongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa asilimia 9 na mahudhurio kwa asilimia 10, huku pia ukisaidia kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa asilimia 20 miongoni mwa watoto wa umri wa kwenda shule.

"Tunaipongeza Tanzania kwa kuendelea kuonesha uongozi katika utekelezaji wa mpango wa chakula shuleni kupitia miongozo ya kitaifa ya lishe shuleni, ushiriki wa jamii pamoja na kuunganisha uzalishaji wa chakula kutoka kwa wakulima wa ndani," amesema.

Naye Mratibu wa Chakula na Lishe kutoka Mkoa wa Njombe, Fadhili Msiru, amesema mkoa huo umefanikiwa katika utekelezaji wa mpango wa utoaji wa chakula mashuleni kutokana na ushirikiano mzuri kati ya jamii, wazazi na Serikali.

Amesema kupitia mpango huo, mahudhurio ya wanafunzi shuleni yameongezeka pamoja na kuboresha hali ya afya na uwezo wao wa kujifunza.
Katika maadhimisho hayo, Serikali pia imewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UNICEF, World Food Programme (WFP), GAIN Tanzania na Sanku kwa mchango wao katika kuunga mkono juhudi za kuboresha lishe na huduma ya chakula mashuleni nchini.

No comments:

Post a Comment