Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kukamilika kwa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na kuifanya kuwa kitovu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ameyasema hayo leo, tarehe 22 Machi 2026, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo Mkoani Kaskazini Unguja.
Ameeleza kuwa changamoto za uchakavu wa Bandari ya Malindi, uhaba wa nishati na gharama kubwa za mafuta zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya kiuchumi, lakini Serikali imejipanga kuzitatua kupitia mradi huo wa kimkakati.
Bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za makontena , kuhifadhi zaidi ya lita milioni sita za mafuta na kuzalisha umeme wa megawati 200, hatua itakayochochea uwekezaji na kupunguza gharama za nishati. Mradi huo wenye thamani ya dola milioni 300 unatarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Katika hatua nyingine, hafla hiyo imeambatana na makabidhiano ya vitalu vya ujenzi wa hifadhi ya kimkakati ya mafuta na gesi vitakavyotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya One Petroleum na Shirika la Bandari la Zanzibar.
Aidha, vitalu vya ujenzi wa bohari za mafuta vimekabidhiwa kwa kampuni za Puma, Gapco na Zanzibar Petroleum (ZP) zitakazohamishia miundombinu yao Mangapwani.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi waliopisha mradi huo kuwa watapatiwa stahiki zao kwa haki, huku akiwapongeza kwa ushirikiano wao katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.











No comments:
Post a Comment