SERIKALI YAENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA BARRICK-TWIGA KWA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZAKE KWA WELEDI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 24, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA BARRICK-TWIGA KWA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZAKE KWA WELEDI

 



Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi wa Mashirika na makampuni ambayo serikali ina hisa chache kwenye mkutano wa mwaka 2026 uliyofanyika jijini Arusha , waliosimama wa kwanza kulia , ni Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi wa Mashirika na makampuni ambayo serikali ina hisa chache kwenye mkutano wa mwaka 2026 uliyofanyika jijini Arusha , waliosimama wa kwanza kulia , ni Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido.
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) kwenye mkutano huo.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.

**
Serikali imeendelea kutambua mafanikio yanayoendelea kupatikana kutokana na ubia baina ya kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga ambapo katika mkutano wa Wakurugenzi wenye Hisa chache za Serikali (MIF 2026) uliomalizika jijini Arusha imetunukiwa tuzo ya mshindi katika kipengele cha uwakilishi bora wa Bodi za Wakurugenzi (MIF) Directors Forum 2026 Outstanding Board Representation) na ofisi ya Msajili wa Hazina.

Barrick -Twiga imekuwa kinara wa kuendesha shughuli zake kwa kufuata  sheria za madini , kanuni za nchi na kwa uwazi ambapo imefanikisha kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini nchini kwa mafanikio sambamba na kuweza kuchangia Pato la Taifa na kunufaisha wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia  migodi yake ya North Mara,Bulyanhulu na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa.

Mkutano huo uliowakutanisha wakurugenzi wa Bodi,Watendaji Wakuu,Watunga sera na wataalamu mbalimbali ulikuwa jukwaa la kujadili changamoto za uendeshaji na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji wa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.

Katika mkutano huo ,Meneja Mkazi wa Barrick nchini,Dkt. Melkiory Ngido, alifanya wasilisho kuhusu kufikiri upya uendeshaji wa shughuli za madini kwa manufaa katika kipindi hiki cha mpito cha kimkakati katika sekta ya madini sambamba na kuwa na mifumo imara inayoweza kutekelezeka katika siku za usoni  na inayoweza kusimamiwa kwa ufasaha na viongozi wa bodi.

Katika kipengele cha mabadiliko katika mazingira ya uchimbaji madini nchini aligusia masuala mbalimbali ya kuangalia kwa umakini kama vile mahitaji, siasa za kijiografia, umakini katika hatua mbalimbali kwenye tasnia kama vile kwenye uchimbaji na usindikaji na bei tete za bidhaa.

Pia aligusia masuala ya mnyororo wa thamani, kuongeza mauzo ya nje ,udhibiti  wa biashara, kukidhi matarajio ya jamii kunufaika na shughuli za madini na kukidhi mahitaji ya wawekezaji.

Kuhusu suala la kufikiri upya undeshaji wa shughuli za madini kwa manufaa aligusia masuala ya athari zinazoweza kujitokeza katika uwekezaji katika tasnia ya madini nchini ikiwemo kubadilisha kanuni, kukithiri kwa uanaharakati, upotoshaji wa taarifa, siasa za kikanda na masuala endelevu.

Dkt. Ngido aligusia suala la kuimarisha mifumo kama vile kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, huduma za maji na umeme,huduma za kimtandao ,kukuza mnyororo wa thamani wa kimataifa, teknolojia na umuhimu wa kuwa na uongozi unaotoa maamuzi kwa haraka ,kuchochea ukuaji, kujenga uaminifu na kutatua matatizo kwa haraka.

Alisema katika uendeshaji wa shughuli za madini kwa weredi baadhi ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa aliyataja kuwa ni utekelezaji wa malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, kushirikiana na wadau wa nje wenye utaalamu zaidi, kushirikisha jamii, kuweka wazi mgawanyo wa mapato, kuimarisha miundombinu, huduma za umeme na jinsi ya kurithishana ujuzi na kujenga kizazi cha wataalamu wa siku zijazo.

Kuhusu matarajio ya baadaye yanayopaswa kutazamwa katika uboreshaji wa sekta ya madini Dkt. Ngido alisema ni sera, kanuni, sheria masharti ya kutoa leseni , maslahi ya taifa, kuaminiana na kuwa na mawasiliano mazuri na taratibu nzuri za utatuzi wa migogoro.

Akihitimisha wasilisho lake katika mkutano huo, Dkt. Ngido alisema kuna umuhimu wa kuwa na mifumo katika migodi kwa njia ya uwazi,nidhamu na ushirikiano thabiti na mifumo hiyo isiwekwe kwa njia ya dharura.

Akiongea katika mkutano huo,Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu alisema ofisi yake itaendelea kuhakikisha kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zinaendeshwa kwa ufanisi, zinatoa faida endelevu na zinachangia kikamilifu katika ajenda ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.

No comments:

Post a Comment